2014-11-13 14:58:33

Papa : Ufalme wa Mungu u ndani mwetu


Ufalme wa Mungu hukua kila siku ndani mwa Wale wanao ushuhudia kimyakimya bila kelele, wakisali na kuuishi imani yao mahali pote, ndani ya familia, kazini,mashambani na katika mikutano na kukutana wengine, alieleza Papa Francisko, mapema asubuhi Alhamisi, wakati akiongoza Ibada ya Misa katika katika Kanisa dogo Mtakatifu Marta, Vatican.

Katika homilia yake, Papa aliutaja ukimya huo kwamba ni muhimu hata pale kunapokuwa na kupungukiwa au kuishiwa mahitaji muhimu ya mwili, akisema, inaweza kuwa kimebaki kibaba kimoja hadi mwisho wa mwezi, lakini iwapo daima kuna maombi, huduma kwa watoto na wazee, ndani ya nyumba hiyo mna ufalme wa Mungu.Papa anasema, mMbali na kelele za watu, ufalme wa Mungu huwa na njia zake katika kukua, kama inavyokua mbegu iliyofukiwa chini ya aridhi bila ya kuwa na kelele huchipuka na kukua kwa kuvutia.

Homilia ya Papa Francisco, ililenga zaidi katika somo la Injili ya Siku kutoka Mt. Luka, ambapo Yesu anawajibu waliotaka kujua lini Ufalme wa Mungu atakuja. Yesu anajibu, siku itakuja watakapo waambia "huyu hapa au yuko kule ,msiende na wala msiwafuate wao.

Papa Francis alisema Ufalme wa Mungu si tamasha. Kwa wengi hufananisha ufalme wa Mungu kwamba itakuwa ni tamasha kubwa. Papa alibainisha kwamba, pamoja na ujio wa Ufalme wa Mungu kuwa ni sherehe kubwa, sherehe hiyo ni tofauti. Kwa hakika ni sherehe nzuri. Sherehe kubwa. Na Mbinguni itakuwa sherehe, lakini si tamasha. Bahati mbaya , udhaifu wa binadamu hupendelea zaidi matamasha

Papa aliendelea na mafundisho yake kwamba, kwa mara nyingi ya Ibada hugeuzwa kuwa kama matasha ya harusi ambako watu wanapenda kuvaa vizuri mitindo mipya kwa dhamira za kujionyesha wakati wa kupokea Ekaristi. Huo ni ubatili, kwa kuwa Ufalme wa Mungu umo katika kimya cha ndani ambamo hupata kukomaa kimyakimya , bila kujionyesha. Roho Mtakatifu huulisha moyo kupitia nia zake, katika udogo ulioandaliwa vyema kiroho. Na kwa kunukuu maneno ya Yesu Papa alisema, siku itakuja ambapo Ufalme utakuwa wazi kwa nguvu zake zote, na huo utakuwa ukamilifu wa nyakati.
Siku ambayo yeye atapiga mbiu ,na kutoa mwanga kama radi , mwanga utakao mulika kama taa ya umeme juu angani kutoka upande mmoja hadi mwingine. Hivyo ndivyo Mwana wa Mtu katika siku hiyo atakavyo piga kelele. Papa alieleza kwa kuyaelekeza mawazo kwa familia nyingi zenye kudumu katika uvumilivu , zile zinazohangaikia kuidumisha familia , wake kwa waume , wanaohudumia watoto, wajukuu hufika mwisho wa mwezi bila hata ndululu ya fedha iliyobaki katika mfuko wao lakini watu hawa hawakupunguza sala na maombi yao kwa Kristo, Mwana wa Ufalme wa Mungu. Katika familia hizo , kuna Ufalme wa Mungu uliofichika katika siri ya maisha ya kila siku , kila siku ni siku ya takatifu, kwa sababu Ufalme wa Mungu si mbali nao.


Papa Francis iliendelea kueleza kwamba,, hata katika mateso, na msalaba wa maisha ya kila siku - msalaba wa kazi, familia, na mambo mengine ya kijamii ni kutenda mema kimyakimya bila kujionyesha, kwa kuwa msalaba ni sehemu ya Ufalme wa Mungu.

Papa Francisco, alihitimisha na wito kwa wote,ambamo ameomba kuzidisha sala na maombi,kumwomba Bwana, neema ya kukua ndani ya Ufalme wa Mungu, ndani mwetu, kwa ibada, huduma ya upendo, ukimya.


Ufalme wa Mungu ni mnyenyekevu, kama mbegu ilivyokuwa na wa kukaa aridhi na baadaye kukua ndivyo ulivyo unyenyekevu wa roho ,uliosimikwa kwenye nguvu ya Roho Mtakatifu . Na hivyo,Papa akasema, ni juu ya kila mtu kuruhusu kukua katika neema ya ufalme wa Mungu bila majingambo ya kujionyesha kwa mbwembwe, lakini ni kuwa na mabadiliko ya kiroho yanayo tanguliza mbele ukimya, amani, utulivu, katika kuwa karibu wa Mwenyezi Mungu, na wengine, katika ibada kwa Mungu, bila tamasha .








All the contents on this site are copyrighted ©.