2014-11-13 07:49:25

Iweni ni vyombo vya Injili ya matumaini kwa Watu wa Mungu


Watawa wanahamasishwa na Mama Kanisa wakati huu kutoka ili kuuona ukweli wa mambo badala ya kujifungia katika nyumba zao za kitawa; wanapaswa kutoka ili kusikiliza na kujibu kilio cha damu pamoja na mahangaiko ya watu wanaowazunguka; wanahimizwa kutoka ili kuisindikiza Familia ya binadamu katika hija ya maisha yake hapa duniani, kwa kutambua kwamba, wao kama watawa wanapaswa kuwa ni alama wazi ya Injili ya Matumaini kwa Watu wa Mungu. RealAudioMP3

Haya ndiyo yaliyojiri wakati wa maadhimisho ya mkutano mkuu wa hamsini na tatu wa wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume nchini Italia, uliohitimishwa hivi karibuni kwa kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko, aliyekazia pamoja na mambo mengine: umuhimu wa kuonesha ushuhuda wa kinabii unaofumbatwa katika Mashauri ya Kiinjili, kama alivyofundisha na kuishi Yesu mwenyewe kwa watu wa nyakati zake.

Watawa waoneshe mshikamano wa udugu na upendo; wajenge moyo wa toba na wongofu wa ndani kwa kusimika maisha yao katika Neno la Mungu, Sala na Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu, ili kuzungumza kwa kina na Yesu anayejificha katika maumbo ya Mkate na Divai.

Mkutano wa wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume uliokuwa unaongozwa na kauli mbiu “Utume wa Kanisa na Maisha ya Kitawa mintarafu Waraka wa kichungaji uliotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Injili ya Furaha. Maisha ya kitawa yanahitaji kwa namna ya pekee majiundo endelevu yanayopyaishwa na upendo unaosimikwa katika mshikamano na maisha ya kidugu, unaowawajibisha watawa kuwaendea wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kutokana na hali yao ya maisha: kiroho na kimwili. Lengo ni kuwaonjesha Injili ya Furaha na Matumaini yanayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake.

Watawa wanawajibika kuwaendea watu ambao wanakabiliana na majanga katika maisha yao, ili kuwasikiliza kwa makini, ili kuwaganga na kuwaponya; kuwapenda na kuwathamini; kuwaokoa na kuwaojesha matumaini mapya. Watawa wanatambua ugumu na changamoto iliyoko mbele yao, lakini hata hivyo bado wanathubutu kutoka kifua mbele ili kuwatangazia Watu wa Mataifa Injili ya Furaha.

Askofu mkuu Josè Rodrigues Carballo, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za kitume, amekazia mambo makuu matatu: kwanza ni kwenda, pili kuishi na tatu ni kuvuka mipaka. Watawa wawaendee watu ili kujenga umoja na mshikamano wa kitawa, huku wakilitafakari Neno la Mungu na kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa.

Watawa waishi kwa kushuhudia ukweli unaojikita katika uwazi, upendo wa dhati pasi na unafiki, majadiliano yanayoheshimu na kuthamini utu wa mtu; mang’amuzi mapana kwa kuonesha utambulisho na mshikamano wao wa dhati unaowachangamotisha kujisadaka bila ya kujibakiza, kwa ajili ya Mungu na jirani.

Watawa wajitambue kwamba, wao ni vyombo vya haki, amani na upatanisho, daima wajitahidi kutafuta mafao ya wengi bila ya kujitafuta na kujihurumia wenyewe. Watawa waoneshe moyo wa upendo na ukarimu kwa maskini na wote wanaohitaji msaada wa hali na mali.

Askofu Nunzio Galantino, Katibu mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, akizungumza na Wakuu wa Mashirika ya kitawa na kazi za kitume, amewataka watawa kuzama katika uhalisia wa maisha ya watu wanaowahudumia, kwa kuwapokea jinsi walivyo na pale inapowezekana wajifunze kutoka kwao, kwa kuwashirikisha utakatifu wa maisha unaotoa harufu yenye mvuto na mashiko katika huduma kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Kwa njia hii anasema Askofu Galantino, Mashirika ya kitawa na kazi za kitume yanaweza kuwa kweli, ni maabara ya binadamu wapya, watu wenye uwezo wa kutoa maisha yao kwa ajili ya huduma kwa jirani zao bila ya kujibakiza; kwa kuonesha moyo wa upendo na ukarimu; furaha na udugu. Maisha ya kijumuiya hayana budi kujikita katika mshikamano wa kidugu na mapendo yanayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya kila siku; kwa kuheshimu na kuzingatia karama na kanuni za Shirika bila kumezwa na malimwengu, bali yote yawe ni kwa ajili ya sifa na utukufu wa Mungu na binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Watawa wanahamasishwa na Mama Kanisa kujifunza kwa bidii Waraka wa kitume wa Baba Mtakatifu Francisko ili kuweza kuwahudumia watu kwa unyenyekevu, upole na mapendo makuu, kama kielelezo cha Kanisa na wadau katika mchakato wa Uinjilishaji, kwa kuwahudumia na kuwaganga wale waliovunjika moyo.

Watawa wawe na ujasiri wa kumwilisha karama xa mashirika yao bila woga; kwa kushikamana na watu katika kumwilisha Mashauri ya Kiinjili; ili watu waonjeshe huruma na upendo wa Mungu kwa njia ya Mashirika ya Kitawa na Kazi za kitume. Watawa watambue kwamba, mtu jasiri anathubutu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.