2014-11-12 15:16:09

Vyeo katika maisha yaliyowekwa wakfu ni huduma na zawadi kutoka kwa Mungu


Bwana anaendelea kuliongoza kundi lake kwa upendo kupitia utume wa maisha yaliyowekwa wakfu ni maelezo ya Baba Mtakatifu, mapema Jumatano, wakati akitoa Katekesi yake kwa mahujaji na wageni, waliofika kumsikiliza ndani ya Vatican.

Katika Katekesi hii ameendelea kulizungumzia Kanisa, akisema "kama tulivyoona katika tafakari zilizopita, Bwana anaendelea kulisha kundi lake kupitia huduma ya Maaskofu, akisaidiwa na ,Mapadre na mashemasi. Ni katika wao, Yesu hujionyesha kwa katika nguvu ya Roho wake, inayoendelea kuilisha imani, matumaini na ushuhuda wa upendo. Huduma hizi, hivyo, inakuwa ni zawadi kubwa ya Mungu kwa kila jumuiya ya Kikristo na kwa Kanisa zima" "Viongozi wa kanisa, wao wakiwa ni ishara ya maisha ya uwepo wake na upendo wake", Papa Francisco alieleza na kuhoji, leo hii, ni kipi kinachohitajika kwa wahudumu wa Kanisa ili waweze kuuishi ukweli katika utendaji wa huduma zao?

Papa alitoa jibu katika hoja hiyo kwa kuigawa hotuba yake katika vipengere vitatu. Alianza kwa kutazama barua za kichungaji za Mtume Paulo kwa Timotheo na Tito, ambamo mmezungumzia huduma ya Maaskofu, mapadre na mashemasi, na pia wazee na vijana, akisema kwamba, ni maelezo yanayolenga pia kwa kila Mkristo ndani ya Kanisa. Aliendelea kueleza kuwa maaskofu, mapadre, mashemasi, wao wameitwa daima na wanapaswa kutambuliwa kuwa ni kati waliochaguliwa na kuteuliwa katika kundi la waamini kwa ajili ya huduma za Kanisa.
Papa Francisko aliendelea kubaini kwamba, kama kawaida, pamoja na asili ya sifa yake katika imani na maisha ya kiroho - ambavyo haviwezi kupuuzwa, bado ni maisha yenyewe yaliyotajwa katika hali yake ya kibinadamu kwamba, ni maisha yenye unyofu, uvumilivu, upole, aminifu na fadhila. Papa alirudia kutaja: ukarimu, moyo wa kiasi, uvumilivu, upole, uaminifu na wema wa moyo kuwa ni sarufi msingi kwa kila mtendaji wa kanisa. Hizi ni nguzo msingi kwa kila Askofu, kila Padre na kila shemasi. Kwa kuwa, bila nguzo hizi kutumika ni vigumu kuwa na kukutana katika ukweli wa majadiliano, mawasiliano na mahusiano na watu wa Mungu, wake kwa waume, katika namna za kuheshimiana na kuhudumia kwa furaha, uaminifu na ushuhuda.

Papa aliendelea kuweka bayana kwamba, Mtume Paulo kimsingi anapendekeza kwa wanafunzi wake, na hivyo kwa wale wote ambao wamejiweka katika huduma ya uchungaji, yaani maaskofu, mapadre, au mashemasi, akiwahimiza waendelee kupokea na kufanya upya utume wao kama zawadi ya Kinabii waliyo pokea kwa kuwekewa mikono na wazee.(tazama 1 Tim 4:14; 2 Tim 1.6). Hii ina maana lazima kutambua kwamba, vyeo au daraja walililopokea, iwe Uaskofu au Upadre au Ushemasi si kwa sababu wao ni nadhifu zaidi au wenye karama zaidi au ni bora kuliko wengine. Lakini daraja limetolewa kwao, ni tu kwa mujibu wa zawadi, zawadi ya upendo uliotolewa na Mungu katika nguvu Roho wake, kwa manufaa ya watu wake.

Papa anasema, kufahamu hili ni muhimu sana na ni neema inayotakiwa kuonyeshwa katika maisha ya kila siku! Kwa kweli, mchungaji anayefahamu vyema kwamba utume wake ameupata kama zawadi na ni huruma na roho wa Mungu kamwe hawezi kuichukulia kazi yake ni mamlaka makubwa , yanayompa majigambo ya kugandamiza wengine wote chini ya miguu yake, au kuifanya jamii kama ni mali yake au ni ufalme wake binafsi.H

Hivyo ni kuwa na utambuzi yakinifu kwamba, utume ni zawadi , yote ni neema kwa ajili ya katika kazi za kichungaji na pia kwa ajili ya kusaidia kutoanguka katika majaribu na hali za kujisikia kama umekamilika mwenyewe. Ni majaribu ya ubatili, kujitosheleza, kiburi na ufahali. Papa anasema, ole wake Askofu, Padre au shemasi, anayedhani anajua kila kitu, daima kuwa mtu wa kujiona ndiye mwenye jibu sahihi kwa kila kitu na hakuna haja ya kuwa na mtu mwingine. Inapaswa kuwa kinyume chake, dhamira ya kwanza ikiwa ni lazima kukumbuka huruma na upendo wa Mungu, kuwa ndiyo utume wa kwanza wa kanisa unaotakiwa ujionyeshe kwa utiifu na unyenyekevu katika kukutana na kuwaelewa wengine.
Papa anasema ni lazima daima kumshukuru Bwana, kwa sababu katika utu wa mtu na katika utume wa Maaskofu , Mapadre na Mashemasi, tunaendelea kuona na kuliunda Kanisa na kukua katika njia ya utakatifu. Wakati huo huo, sisi ni lazima kuendelea kuomba, ili kwamba, Wachungaji katika jumuia zetu waweze kuwa mfano hai wa katika maisha ya ushirika na upendo wa Mungu.

Baada ya Katekesi, Papa alisalimia kwa lugha mbalimbali kulingana na lugha za makundi makubwa yaliyohudhuria Katekesi hii. Akisalimia kwa Kiitaliano,aliwataja Masista Wascalabriani , Wamisionari Wakarmelite wa Matakatifu Tereza wa Mtoto Yesu ,ambao wako katika Mkutano wao Mkuu. Na pia wanafunzi na walimu kutoka Idara ya sayansi ya Mawasiliano katika Chuo kikuu cha Kipapa cha Salesiani, ambacho kinaadhimisha miaka 25 ya kuanzishwa kwake. Vivyo hivyo alitoa salaam kwa makundi ya kijamii, watoto, vijana,wazee na wagonjwa.

Na kwa namna ya Kipekee, alitoa ombi kwa viongozi wa kimataifa na kitaifa na mahalia pia, kuchukua kila tahadhari kwenye hatua za kulinda raia na msaada kwa Wakristo wanaoteseka katika sehemu mbalimbali za dunia. Alieleza hilo huku akionyesha ukaribu wake kwa watu wa Mexico kwa janga la kupotea kwa kundi la wanafunzi, wanaodaiwa kuuawa na wafanya biashara haramu ya madawa ya kulevya. Na alikumbuka maadhimisho ya miaka 30 ya mkataba wa amani kati ya Argentina na Chile, akirejea mazungumzo yaliyo fanikisha amani kwa watu wote na hivyo vita kusitishwa. Mwishi kwao wote aliwapa baraka zake za Kipapa.







All the contents on this site are copyrighted ©.