2014-11-12 09:08:06

Kanisa linakazia: tunu msingi za maisha ya ndoa na familia na uhuru wa kuabudu!


Yaliyojiri katika maadhimisho ya Sinodi maalum ya Maaskofu kwa ajili ya familia iliyofanyika mjini Vatican kuanzia tarehe 5 hadi tarehe 19 Oktoba 2014; maandalizi ya Siku ya Familia Kimataifa itakayoadhimishwa katika Jimbo kuu la Philadelphia, Marekani, mwaka 2015; uhuru wa kidini na umuhimu wa Kanisa kusimama kidete kulinda na kutetea tunu msingi za maisha ya ndoa na familia ni kati ya mambo msingi yaliyojitokeza wakati wa mkutano wa Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani.

Maaskofu wamepembua mikakati ya kichungaji kwa ajili ya mchakato wa Uinjilishaji mpya, kwa kujikita katika maadhimisho ya Ibada na Ushuhuda wa imani tendaji, pamoja na kuwasaidia watu wanaoishi pembezoni mwa Jamii kupata mafundisho ya Kanisa Katoliki.

Mkutano huu umefunguliwa kwa hotuba iliyotolewa na Askofu mkuu Carlo Maria Vigano', Balozi wa Vatican nchini Marekani aliyekazia umuhimu wa Kanisa kuendelea kutembea pamoja na Familia katika furaha, shida na changamoto wanazokabiliana nazo kila siku, ili kwa kuonjeshwa huruma na upendo unaobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake, Familia ya binadamu iweze kuwa na matumaini pamoja na kutekeleza dhamana na utume wake ndani ya Kanisa.

Ni wajibu wa Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, Familia zinaendelea kustawi katika imani, matumaini, mapendo na mshikamano wa dhati; mambo msingi yanayoziwezesha kudumu, huku wakiwa wanaambatana na Yesu Kristo kwa njia ya ushuhuda wa imani tendaji. Kanisa ni kielelezo cha huruma na upendo wa Mungu; hapa anasema Baba Mtakatifu Francisko ni mahali ambapo waamini wanaweza kujichotea huruma na kuonjeshwa ukarimu, upendo, msamaha pamoja na kuhamasishwa kuishi maisha mema kadiri ya tunu msingi za Kiinjili.

Maaskofu Katoliki Marekani wanasema, Famili za Kikristo hazina budi kufundwa mintarafu: Maandiko Matakatifu, Mapokeo ya Kanisa pamoja na mang'amuzi ya wanandoa na familia bila kusahau mchango unaotolewa na wachungaji wa Kanisa; ili kweli Familia ziweze kukabiliana na changamoto zinazoendelea kujitokeza katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Familia zinahamasishwa kusali na kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa kwa umoja, ili kweli Familia ziweze kuwa ni Kanisa dogo la nyumbani.

Maaskofu wanasema, Maadhimisho ya Siku ya Familia Kimataifa huko Philadelphia, itakua ni fursa kwa Mama Kanisa kusikiliza, kuzungumza, kusali na kutafakari pamoja na wanandoa kutoka sehemu mbali mbali za dunia, kwa matumaini ya uwepo wa Baba Mtakatifu Francisko; ili kweli Familia ziweze kuendelea kuwa ni wajumbe wa furaha na walinzi wa tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, kwa kung'ara zaidi na zaidi katika uaminifu kwa Injili ya Kristo.

Ni wajibu wa Familia kuendelea kutangaza Injili ya Uhai kwa kukataa kishawishi cha kukumbatia utamaduni wa kifo, kama njia ya kulinda utu na heshima ya binadamu.

Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani linamshukuru Mungu kwa kuwawezesha kwa njia ya mshikamano wa upendo kuwatangazia Watu wa Mataifa Injili ya Furaha, hasa wale walioathirika kutokana na majanga asilia na wale wanaoendelea kudhulumiwa na kunyanyaswa kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Mchakato wa Uinjilishaji maana yake ni kushuhudia imani, matumaini na mapendo kwa Kristo na Kanisa lake, katika hali ya unyenyekevu, imara na thabiti katika umoja na mshikamano.

Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani Mwaka 2015 litaadhimisha Jubilee ya Miaka 50 tangu Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican walipochapisha Tamko kuhusu uhuru wa kidini, yaani "Dignitatis Humanae"; msingi mkuu katika mahusiano kati ya watu; uhuru wa mtu kutenda kadiri ya imani yake pamoja utume wa Kanisa katika masuala ya uhuru wa kuabudu. Huu utakuwa ni wakati muafaka wa kufundisha umuhimu wa uhuru wa kidini pamoja na kuendelea kuinjilisha.

Ili kukabiliana na changamoto, matatizo na fursa katika maisha ya ndoa na Familia, Maaskofu hawana budi kutoka kifua mbele, kwa kufuata mfano wa Baba Mtakatifu Francisko ili kujenga utamaduni wa watu kukutana, kwa kuwangoza kikamilifu wanandoa katika mapito ya maisha kwa imani, matumaini na mapendo pamoja na kuendelea kukazia ushuhuda wa tunu msingi za maisha ya ndoa na familia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.