2014-11-12 11:24:21

Kampeni dhidi ya nyanyaso na ukatili wa majumbani nchini Uganda


Askofu mkuu John Baptist Odama, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Uganda anasema, Kanisa Katoliki Uganda tangu mwaka 2010 kwa kushirikiana na wadau mbali mbali limekua likiendesha kampeni dhidi ya nyanyaso na ukatili majumbani, ili kukuza na kudumisha: usalama, amani na utulivu ndani ya familia na jamii kwa ujumla.

Kampeni hii ambayo imezinduliwa hivi karibuni kwa mwaka huu, inapania kuwaelimisha wananchi madhara ya nyanyaso na ukatili wa majumbani ili watu waweze kubadili tabia na kuwa wema zaidi. Kampeni hii inadumu kwa kipindi cha mwaka mzima, lakini mkazo unawekwa zaidi wakati wa Kipindi cha Majilio, wakati waamini wanapojiandaa kwa ajili ya kuadhimisha Fumbo la kuzaliwa kwa Yesu Kristo Mkombozi wa dunia.

Mwaka huu anasema Askofu mkuu Odama, Kampeni hii inaanza rasmi hapo tarehe 30 Novemba 2014, kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuungana kwa pamoja katika sala pamoja na viongozi kuhamasisha waamini na watu wenye mapenzi mema kuachana na tabia ya ukatili na nyanyaso za majumbani. Familia nchini Uganda linahimizwa kusali kwa ajili ya kuombea amani na utulivu, kwa kushiriki kikamilifu katika kupambana na vitendo vyote vinavyosababisha nyanyaso na ukatili wa majumbani.

Kampeni ya Mwaka huu inaongozwa na kauli mbiu "Ushirikishwaji wa maamuzi, maendeleo na furaha". Kwa kufanikisha mchakato huu, Familia zinazoishi na kusali pamoja zitaweza kutokomeza nyanyaso na ukatili wa majumbani. Baraza la Maaskofu Katoliki Uganda linawaalika waamini na wananchi wote katika ujumla wao kuunga mkono juhudi za kupambana na vitendo hivi vinavyodhalilisha utu na heshima ya binadamu, ili kujenga na kudumisha misingi ya amani, furaha na upendo.







All the contents on this site are copyrighted ©.