Askofu mkuu Telesphore Mpundu wa Jimbo kuu la Lusaka, Zambia wakati wa Ibada ya mazishi
ya Rais Michael Chilufya Sata yaliyohudhuriwa na umati mkubwa wa wananchi kutoka ndani
na nje ya Zambia, Jumanne tarehe 11 Novemba 2014, amewataka wanasiasa nchini Zambia
kuhakikisha kwamba wanadumisha na kukuza umoja na mshikamano wa kitaifa, hasa wakati
wa kampeni za kuwania kiti cha Urais.
Ni wajibu wa Serikali ya mpito kuhakikisha
kwamba, uchaguzi mkuu unakuwa: huru, haki na uwazi, ili kuwawezesha wananchi wa Zambia
kutekeleza wajibu wao wa kikatiba.
Rais Sata aliyefariki dunia huko London,
Uingereza tarehe 28 Oktoba 2014 amezikwa kwenye Uwanja wa Mabalozi mjini Lusaka na
umati mkubwa wa waombolezaji wamefuatilia tukio hili kwa simanzi na majonzi makuu.
Askofu mkuu Mpundu amewataka wanasiasa kuiga mfano bora wa Marehemu Rais Sata ambaye
katika chaguzi mbali mbali nchini Zambia alishindwa mara tatu, lakini hakukata tamaa
wala kuingia "porini" kutafuta madaraka kwa matumizi ya nguvu. Wakati wa kampeni,
wanasiasa wauze sera na mikakati inayopania kuwaletea wananchi wa Zambia ustawi na
maendeleo endelevu yanayogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.
Askofu
mkuu Mpundu anasema, Zambia kwa sasa inahitaji mambo makuu mawili: mshikamano wa kitaifa
na amani; mambo msingi yatakayowawezesha kupambana na umaskini wa hali na kipato,
ili kuboresha maisha yao zaidi. Wanasiasa na vijana wajifunge kibwebwe ili kufanya
kazi kwa tija na ufanisi mkubwa kwa ajili ya watu wao kabla ya kuanza kutamani madaraka
makubwa!