2014-11-11 07:57:53

Wanawake ni majembe ya kazi katika maisha na utume wa Kanisa! Lakini...!


Baraza la Maaskofu Katoliki Ufaransa katika mkutano wake mkuu wa mwaka, uliohitimishwa Jumapili tarehe 9 Novemba 2014 pamoja na mambo mengine, limejadili kwa kina na mapana kuhusu dhamana na nafasi ya wanawake katika maisha na utume wa Kanisa kwa kutambua uwezo na mchango wao katika ustawi na maendeleo ya Kanisa.

Kwa wanawake kutopewa Daraja Takatifu la Upadre si kwamba, wamefungiwa mlango wa ushiriki wao katika maisha na utume wa Kanisa. Mchango wa wanawake unatambuliwa na Kanisa, kwani mahusiano msingi kati ya mwanaume na mwanamke yanawasaidia kukamilishana kadiri ya mpango wa Mungu.

Kanisa linataka kuona ushuhuda makini unaotolewa na wanawake na wanaume, walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, lakini kwa bahati mbaya, ushuhuda unaotolewa na wanawake ndani ya Kanisa haujathaminiwa sana, kutokana na mfumo dume kutawala kwa kiasi kikubwa katika maisha na utume wa Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kichungaji, Injili ya Furaha anatambua mchango mkubwa unaotolewa na wanawake katika maisha na utume wa Kanisa.

Wanawake wanashirikisha wito na karama zao katika mikakati mbali mbali ya shughuli za kichungaji; ni watu wanaojisadaka kwa kiasi kikubwa katika kuwasaidia watu kwa hali na mali, changamoto kwa Kanisa kujikita katika tafiti za kitaalimungu ili kubainisha mchango unaotolewa na wanawake kwa nyakati hizi. Wanawake wanapaswa pia kushirikishwa katika mikutano inayopanga na kutekeleza maamuzi mbali mbali katika maisha yao ya kila siku, ili waweze kutoa ushuhuda wa Kiinjili, ambao mara nyingi una mashiko na mguso mkubwa.

Baraza la Maaskofu Katoliki Ufaransa linasema kwamba, Mapadre hawana budi kusaidia malezi ya miito mbali mbali ndani ya Kanisa kwa kutoa pia nafasi kwa wanawake kushirikisha karama na vipaji vyao katika maisha na utume wa Kanisa. Wanawake wapewe nafasi na madaraka kadiri ya uwezo wao na kamwe wasibaguliwe kutokana na kukithiri kwa mfumo dume ndani ya Kanisa. Wanawake ni watu ambao wanauwezo mkubwa katika mang'amuzi yao; wanaweza kusikiliza kwa makini pamoja na kujadiliana kwa kina na mapana.

Mawazo na mchango wa wanawake katika maisha na utume wa Kanisa vinapaswa kuthaminiwa, changamoto endelevu kwani si rahisi kuvunjilia mbali mfumo dume ambao umeota mizizi ndani ya Kanisa kwa miaka mingi wanasema Maaskofu Katoliki wa Ufaransa. Huu si wakati kwa wanawake kulipiza kisasi, bali kuhakikisha kwamba, mchango wao unatambuliwa na Kanisa, kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Familia ya Mungu katika ujumla wake!







All the contents on this site are copyrighted ©.