Tanzania kuyakingia kifua makabila madogo madogo ili yasitoweke!
Waziri mkuu wa Tanzania Mizengo Pinda amesema Serikali yake itaendelea kuyalinda makabila
madogo nchini yakiwemo ya Wahdazabe na Wasandawe ambayo yanategemea rasilmali misitu
kwa maisha yao na ustawi wao. “Tutakuwa tunafanya makosa kama tutawanyang’anya rasilmali
misitu makabila madogo hapa nchini kama vile Wahadzabe, Wandorobo na Wasandawe kwani
ndiyo rasilami pekee inayowawezesha wapate chakula cha kutosha,” alisema. Ametoa
kauli hiyo Jumanne, Novemba 11, 2014 wakati akifungua Kongamano la Kwanza la Ufugaji
Nyuki Barani Afrika la Mwaka 2014 lililoanza rasmi kwenye ukumbi wa AICC, jijini Arusha.
Kongamano hilo linashirikisha wajumbe 590 kutoka ndani na nje ya nchi. Nchi za nje
zinazoshiriki kongamano hilo ni 24, ambapo kati ya nchi hizo nchi 12 ni za bara la
Afrika. Kongamano hilo la siku tatu limeandaliwa na Wizara ya Maliasili na Utalii
kwa lengo la kuwakutanisha wafugaji nyuki, wafanyabiashara, wataalamu na wawakilishi
wa taasisi za ndani na nje ya nchi ili kujadili njia za kuboresha ufugaji nyuki na
kukabiliana na changamoto za ufugaji nyuki hapa nchini na barani Afrika kwa ujumla. Waziri
Mkuu aliwataka viongozi wa Halmashauri na watu wenye maamuzi wasiwasumbue kwa kuwalazimisha
wabadili maisha yao na kutoka kwenye mfumo wa ikolojia (ecosystem) ambao wameuzoea.
“Tusiwabugudhi, tusiwatoe kwenye mfumo wao wa ikolojia. Tuwasaidie kuwapa teknolojia
mpya ili waweze kufuga kisasa na kupata faida huku wakiishi kwenye mazingira hayohayo
waliyoyazoea mpaka hapo watakapozoea na kuamua kubadilika kwa kubaini kuwa njia zao
za zamani haziwasaidii sana.” Akizungumzia kuhusu ufugaji nyuki barani Afrika,
Waziri Mkuu alisema ufugaji nyuki umeegemea zaidi katika rasilimali misitu na kilimo
ambapo Afrika kwa asilimia kubwa shughuli ya ufugaji nyuki hufanyika katika misitu.
“Bara la Afrika lina ukubwa wa eneo la kilometa za mraba milioni 30.2 na asilimia
20 ya eneo hilo ni misitu. Asilimia 40 ni misitu ya Savanna ambayo ni muhimu kwa ajili
ya ufugaji nyuki. Mapori haya pamoja na maeneo ya kilimo yana uwezo mkubwa wa kuzalisha
mazao ya nyuki kwa wingi,” alisema Waziri Mkuu. Akizungumzia kuhusu ufugaji nyuki
nchini Tanzania, Waziri Mkuu alisema takwimu za Shirika la Chakula la Umoja wa Mataifa
(FAO) zinaonesha kuwa Tanzania ni nchi ya pili barani Afrika inayozalisha asali kwa
wingi (tani 34,000 kwa mwaka), ya kwanza ikiwa ni Ethiopia (tani 45,000 kwa mwaka). “Inakadiriwa
kuwa Tanzania ina uwezo wa kuzalisha tani 140,000 za asali na tani 10,000 za nta kwa
mwaka. Lakini ni asilimia saba tu ya uwezo huo ndio huzalishwa. Hii ni kwa sababu
zao hilo limepuuzwa tangu siku nyingi na halijapewa msukumo unaostahili.” Alisema
sekta ya ufugaji nyuki ina mchango mkubwa katika maisha ya mwanadamu kwa kumpatia
chakula, ajira na kipato. “Wananchi hunufaika kutokana na mauzo ya asali, nta na mazao
mengine ya nyuki, utengenezaji wa vifaa vya ufugaji nyuki, kusambaza malighafi za
viwandani na huduma ya uchavushaji,” aliongeza. “Wafugaji wa nyuki katika nchi
zilizoendelea wanatumia teknolojia ya kuvuna sumu ya nyuki (bee venom), gundi ya nyuki
(propolis), maziwa ya nyuki (royal jely) na chavua (pollen) ambavyo hutumiwa kama
virutubisho na dawa. Tafiti zimethibitisha kuwa gundi ya nyuki hutibu maumivu ya meno,
malaria na homa ya mifupa(arthritis) na kuongeza kinga mwilini. Sumu ya nyuki imekuwa
ikitumiwa kuongeza nguvu za uzazi, kutibu uvimbe na homa ya mifupa,” alisema huku
akishangiliwa. Waziri Mkuu aliitaka sekta binafsi na taasisi za utafiti barani
Afrika zifanye tafiti zaidi katika eneo hili na kuwekeza katika teknolojia ambayo
inaweza kuvuna na kuchakata mazao hayo ambayo yana soko kubwa katika viwanda vya kutengeneza
madawa, virutubisho na vipodozi. Mapema, akielezea kuhusu kongamano hilo, Waziri
wa Maliasili na Utalii, Bw. Lazaro Nyalandu alisema Juni mwaka jana, Wizara hiyo ilisaini
makubaliano na Shirikisho la Ufugaji Nyuki Duniani (Apimondia) ili waweze kuandaa
kongamano la ufugaji nyuki barani Afrika mwaka 2014. Alisema kongamano hilo ambalo
kaulimbiu yake ni: “Kufuga nyuki kwa kuzingatia hifadhi ya mazingira na kukuza uchumi”
yaani “African Bees for a Green and Golden Economy” litahusisha mada 88 ambazo kati
yake, 45 zitawasilishwa na watafiti wa kisayansi, 26 zitakuwa za majadiliano (roundtable)
na 17 zitawasilishwa katika semina. Alisema kongamano hilo ni kwanza kwa sababu
ni mara ya kwanza kwa kongamano kama kuandaliwa barani Afrika kwa kushirikiana na
Apimondia kwa lengo la kubadilishana uzoefu kuhusu species za nyuki zilizopo Afrika
na mazingira ya ufugaji nyuko barani humu.