2014-11-11 11:46:23

Sekuru Michael Chilufya Sata, RIP. Amina!


Viongozi wa Serikali na nchi mbali mbali Barani Afrika, Jumanne tarehe 11 Novemba 2014 wameungana na mamillioni ya wananchi wa Zambia kumsindikiza Marehemu Rais Michael Chilufya Sata katika usingizi wa amani. Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe anasema, Marehemu Rais Sata alikuwa ni mtu wa watu, amefariki dunia huku akiwa na ndoto na mipango mikubwa kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wananchi wa Zambia, ambayo imebaki ikiwa imejikita katika siri ya moyo wake!

Kifo cha Rais Sata ni pigo kubwa si tu kwa Zambia, bali kwa Bara la Afrika kwa ujumla, kwani ni kiongozi aliyejifunga kibwebwe kupambana na baa la umaskini miongoni mwa watu wake.

Katika Ibada ya pamoja kwa ajili ya kumwombea Marehemu Rais Sata, iliyofanyika siku ya Jumatatu, tarehe 10 Novemba 2014 kwenye Ukumbi wa Bunge la Zambia, mjini Lusaka, viongozi mbali mbali wamewataka wananchi wa Zambia katika ujumla wao, kuendelea kuwa na matumaini katika maisha ya uzima wa milele, licha ya majonzi makubwa ambayo kwa sasa wanakabiliana nayo kwa kuondokewa na mpendwa wao, ambaye viongozi wengi Kusini mwa Afrika walipenda kumwita "Sekuru". Waamini wawe na imani katika ufufuko wa wafu kwani Yesu ameshinda mauti na kifo kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake pale Msalabani.

Waamini na viongozi kwa namna ya pekee kabisa wamehamaishwa kukesha na kusali kwani hawajui siku wala saa wanapoweza kukukabiliana na Fumbo la Kifo katika maisha yao. Cheo na madaraka waliyo nayo yasiwe ni sababu ya wao kushindwa kuingia katika maisha ya uzima wa milele, bali madaraka yao yawe ni kielelezo cha huduma makini kwa wananchi, daima wakitafuta mafao ya wengi, ustawi na maendeleo ya wananchi wao.

Viongozi wa Makanisa wanasema, Marehemu Rais Sata alijielekeza zaidi katika huduma kwa wananchi wa Zambia, akampatia Mwenyezi Mungu kipaumbele cha kwanza katika maisha na mipango yake. Viongozi wa Kanisa wanaendelea kusali kwa ajili ya kuombea Zambia wakati huu wa kipindi cha mpito, ili iweze kuonesha mshikamano wa kitaifa, kukuza na kudumisha amani na utulivu.

Mwili wa Marehemu Michael Chilufya Sata aliyefariki dunia tarehe 28 Oktoba 2014 Jijini London, umezikwa kwenye Makaburi ya Viongozi wa Serikali, kwenye Uwanja wa Mabalozi, unaotazamana na Ofisi za Bunge la Zambia.







All the contents on this site are copyrighted ©.