2014-11-11 12:02:45

Mheshimiwa Padre Prosper Balthazar Lyimo ateuliwa kuwa Askofu msaidizi, Jimbo kuu la Arusha, Tanzania


Baba Mtakatifu Francisko amemteua Mheshimiwa Padre Prosper Balthazar Lyimo, kuwa Askofu msaidizi wa Jimbo kuu la Arusha, Tanzania. Askofu mteule Lyimo kabla ya uteuzi huu alikuwa ni Katibu mkuu wa Jimbo na Mkuu wa Mahakama ya Kanisa Jimbo kuu la Arusha.

Askofu mteule Prosper Balthazar Lyimo alizaliwa kunako tarehe 20 Agosti 1964 huko Kyou-Kilema, Jimbo Katoliki la Moshi. Baada ya masomo yake ya shule ya msingi huko Maua na Arusha, alijiunga na Seminari ndogo ya Jimbo Katoliki Arusha. Alipata masomo yake ya Falsafa kwenye Seminari kuu ya Kibosho, iliyoko Jimbo Katoliki la Moshi na masomo ya Taalimungu alipata Seminari kuu ya Kipalapala, iliyoko Jimbo kuu la Tabora.

Baada ya majiundo yake ya Kikasisi, akapadrishwa Jimbo kuu la Arusha kunako tarehe 4 Julai 1997. Tangu wakati huo amekuwa ni mlezi katika Seminari ndogo ya Jimbo kuu la Arusha kuanzia mwaka 1997 hadi mwaka 1999. Kuanzia mwaka 2000 hadi mwaka 2004 alikuwa ni Katibu mkuu wa Jimbo kuu la Arusha. Kunako mwaka 2004 hadi mwaka 2007 alipelekwa na Jimbo kwa ajili ya masomo ya juu mjini Roma, kwenye Chuo kikuu cha Kipapa cha Urbaniana. Kunako mwaka 2007 hadi mwaka 2008 alikuwa ni Katibu mkuu wa Jimbo kuu la Arusha.

Kuanzia mwaka 2008 hadi mwaka 2011 Askofu mteule Prosper Balthazar Lyimo, alitumwa na Jimbo kuu la Arusha kwa ajili ya masomo ya juu nchini Canada na huko akajipatia shahada ya uzamivu kutoka katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Paul, kilichoko mjini Ottawa. Na kunako mwaka 2011 alirejea nchini Tanzania na kupangiwa kazi ya kuwa Katibu mkuu na Mkuu wa Mahakama ya Jimbo kuu la Arusha.







All the contents on this site are copyrighted ©.