Yapyaisheni maisha ya Familia kwa kusoma Nyaraka za Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican!
Mpendwa msikikizaji wa Kipindi chetu cha Kanisa la nyumbani, tumsifu Yesu Kristo!
Kama tulivyokuahidi katika vipindi vilivyopita, karibu tuendelee kushirikiana katika
kuyapyaisha mafundisho ya Mtaguso Mkuu wa II wa Vaticani, ili sote kwa pamoja, kila
mmoja kwa nafasi yake na sote kama familia ya Mungu, tuweze kuuishi mtaguso huo maalumu.
Kabla hatujasonga
mbele, tukumbushane kwa ufupi tu juu ya hati zote za mtaguso huo Mkuu, ili tuone namna
zinavyounganika katika kutupatia ujumbe mmoja. Hati hizo zipo katika makundi makubwa
matatu. Kuna katiba 4, hizi zimesheheni mafundisho ya kiimani zaidi na hivyo zina
hadhi ya ki-nguziimani. Hati ya kwanza inaitwa Sacrosanctum Concilium.
Hati hii inazumgumza juu ya Liturujia Takatifu. Inatuelekeza kuelewa kwa undani zaidi
fumbo la sadaka ya Bwana, ukuu wa Mungu na jinsi tunavyopaswa kumwabudu Mungu. Hati
ya pili kwa kilatini inaitwa Lumen Gentium, maana yake Mwanga wa Mataifa. Hii
inaelezea juu ya fumbo la Kanisa, na inalieleza Kanisa kama Mwanga wa Mataifa. Ya
tatu inaitwa Dei Verbum, maana yake Neno la Mungu. Hii inaielezea juu ya Ufunuo
wa Kimungu. Hati ya nne inaitwa Gaudium et Spes, maana yake furaha na matumaini.
Hii inalielezea Kanisa katika Ulimwengu wa Kisasa. Kundi la pili la hati za Mtaguso,
ni za maagizo mbalimbali. Pamoja na hati za Mafundisho tanzu ya Kanisa, ambazo zinabeba
mafundisho-msingi ya Kanisa, Mababa wa Mtaguso walitoa maagizo ya kuyafuata katika
nyanja mbalimbali za maisha ya Kanisa. Agizo la kwanza linaitwa Inter Mirifica.
Hati hii inaelezea juu ya vyombo vya upashanaji habari. Agizo la pili linaitwa Orientalium
Ecclesiarum. Hati hii inahusu Makanisa Katoliki ya Mshariki. Agizo la Tatu linaitwa
Unitatis Redintegratio, ambayo inaongelea juu ya Uekumene. Agizo la nne linaitwa
Christus Dominus, hii inaelezea juu ya huduma ya kichungaji ya maaskofu. Agizo
la tano linaitwa Perfectae Caritate, inayoongea juu ya kurekebishwa kwa maisha ya
wakfu. Agizo la sita linaitwa Optatam Totius. Hii inaongelea juu ya malezi
ya Kipadre. Agizo la saba linaitwa Apostolicam Actuositatem, hati ambayo inaongelea
juu ya Utume wa walei. Agizo la nane linaitwa Ad Gentes, yaani kwa Mataifa. Ni hati
inayoongelea juu ya utendaji wa Kimisionari wa Kanisa. Agizo la tisa linaitwa Presibiterorum
Ordinis ambayo inaongelea juu ya huduma na maisha ya Kipadre. Kundi la tatu
la hati za Mtaguso ni Matamko. Nayo yapo matatu tu. Tamko la kwanza ni juu ya malezi
ya Kikristo. Mababa walichambua kwa kina sana juu ya suala la malezi katika nyanja
zote. Tamko la pili linaitwa Nostra Aetate. Katika hati hii, mababa wanaangazia
juu ya Uhusiano wa Kanisa na dini zisizo za Kikristo. Na tamko la tatu linaitwa Dignitatis
Humanae, maana yake ni hadhi ya mwanadamu. Ni hati inayozungumzia juu ya Uhuru
wa kidini. Tunazileta hati hizi masikioni mwako mpendwa msikilizaji ili kwa ufupi
tu tupate kukumbushwa mababa wa Mtaguso walitaka Kanisa lieleweke, lionekane na
litende vipi katika hija yake ya hapa duniani. Kwa kuzidonoa kwa umbali hati hizo
zote, leo tuione mmoja tu il ya kwanza ihusuyo Liturujia au utaratibu wa Ibada katika
katika Kanisa Katoliki. Hati hii inaitwa Sacrosanctum concilium. Hati hii ndiyo
iliyoleta mageuzi makubwa katika ibada za kanisa katoliki, hasa matumizi ya lugha
mahalia za watu, badala ya kutumia kilatini kwa Kanisa zima ambacho si wote walikuwa
wanakielewa. Lengo la hati hii ni kutusaidia sisi sote tumwabudu Mungu kama astahilivyo
na sisi wenyewe tupate mafaa ya kiroho. Hati hii pia inasisitiza juu ya malezi
ya kiliturujia maseminarini na katika nyumba za kitawa. Kwa njia hiyo waamini wote
watasaidiwa kuchota roho halisi ya Kikristo katika chemchemi hiyo ya kwanza na ya
lazima; pia wataweza kushiriki ibada kwa ukamilifu wote. Msisitizo wa pekee unapelekwa
katika matendo ya kiibada. Ibada zetu zinatuunganisha sote pamoja kama familia ya
Mungu, na kwa pamoja tunamwinulia Mungu mioyo yetu, naye kama baba yetu sote anatubariki
na kutusikiliza tunapoliitia jina lake kwa pamoja na kwa heshima astahiliyo. Sura
ya pili na ya tatu ya hati hii, inazungumzia juu ya Misa Takatifu, sakramenti na visakramenti,
na sura ya nne inazungumzia juu ya sala ya Kanisa. Sura mbili za mwisho zinaelezea
kwa kinagaubaga juu ya Muziki na sanaa takatifu. Na inaelekeza kwamba, vipawa mbalimbali
vya mwanadamu vitumike katika kumsifu Mungu. Mpendwa msikilizaji, tunataka mtaguso
utue ndani ya familia yako, ndani ya maisha yako. Tunapoitafakari hati hii, wanakanisa
la nyumbani tukumbuke wajibu wetu wa kuiishi liturujia. Wakuu wa liturujia takatifu
katika familia ni baba na mama. Swali tunalojiuliza sisi wanafamilia ni hili: Mungu
mmoja na wa kweli ana nafasi katika familia yetu? Mungu huyo anaabudiwa ipasavyo?
Tunasali kwa pamoja kuliitia jina la Mungu ndani ya familia yetu? Vipaji alivyonavyo
kila mmoja wetu katika familia yetu, vinamtukuza Mungu na kutuletea usitawi sisi wanafamilia?.
Kisha, sisi kama wanafamilia, tunashiriki vipi katika kuboresha Ibada Takatifu
Kanisani? Wanakwaya wanatoka katika familia, wanavyama vya kitume wanatoka katika
familia, wahudumu mbalimbali wa misa wanatoka katika familia. Huwa inatokea bahati
mbaya ya aibu sana pale ambapo wazazi wanawakataza kabisa watoto wao kushiriki katika
mambo ya Kanisa; au wazazi wanakuwa baridi sana katika kuwahimiza watoto wao kwa mambo
ya kiroho. Huko ni kulihujumu Kanisa la Nyumbani na Kaniza zima. Sote kwa pamoja tushiriki
katika kuboresha Ibada zetu na kulinda unadhifu wake. Tunarudia tena neno lile,
familia ni shule ya sala, ni shule ya liturujia msingi. Ndiko tunafundishwa sala na
Ibada na majitoleo kwa watakatifu mbalimbali. Lengo la mabadiliko katika liturujia
ya Kanisa ni kujaribu kuwasaidia waamini wasali pamoja, huku wakielewana kwa lugha
zao za kawaida. Na sisi katika familia zetu tunaomba na kusihi sana, sala za familia,
liturujia ya familia iwe ni chombo cha kuiunganisha familia. Tuwe kitu kimoja, twende
pamoja, tutasafiri kwa amani na kufika salama. Lakini kama kila mtu anaabudu alikogeukia,
hakika mwovu hataacha kutupepeta kila siku. Tusiyapuuzie mambo ya kiroho na mazoezi
yote ya kiroho kwani yana umuhimu mkubwa sana katika kutuunda na kutusindikiza katika
maisha yetu ya kila siku. Hadi wakati mwingine tena.
Kutoka katika studio
za Radio Vatican, ni mimi Padre Pambo Martin Mkorwe, OSB.