Mitandao ya kijamii ni jukwaa makini la Uinjilishaji
Uwepo wa Kanisa katika mitandao ya kijamii ni jambo la muhimu sana katika mchakato
wa majiundo makini ya binadamu katika kukuza mahusiano hasa nyakati hizi za teknolojia
ya digitali. Kanisa linapenda kuwasindikiza waamini na watu wote wenye mapenzi mema
katika hija yao ya maisha, ili kujenga mahusiano yanayojikita katika mshikamano wa
upendo kwa kutambua kwamba, kila mtu ni jirani, kwani ameumbwa kwa sura na mfano wa
Mungu.
Huu si mkakati wa shughuli za kichungaji kwa ajili ya Mama Kanisa,
bali ni sehemu ya utume na dhamana yake kwa binadamu. Mitandao ya kijamii, ina faida
kubwa katika ustawi na maendeleo ya binadamu, lakini pia imekuwa kama dunia ambayo
ni tambara bovu! Mahali ambapo kwa sasa kuna changamoto nyingi za kimaadili na utu
wema.
Pamoja na mapungufu haya yote, Mama Kanisa anatambua kwamba, mitandao
ya kijamii ni Jukwaa makini sana katika kuwatangazia Watu wa Mataifa Habari Njema
ya Wokovu, hadi miisho ya dunia. Haya ndiyo yaliyojitokeza kwa uwazi mkubwa wakati
wa mkutano wa Wakurugenzi wa Idara za Mawasiliano kutoka Shirikisho la Mabaraza ya
Maaskofu Katoliki Ulaya, CCEE, wakati walipokutanika hivi karibuni mjini Athens, Ugiriki,
ili kutafakari kwa pamoja kuhusu mawasiliano kama mahali pa kukutana katika ukweli
na uhalisia wa maisha.
Mkutano huu umehudhuriwa na Maaskofu 40 pamoja na mabingwa
na wataalam wa sayansi ya mawasiliano ya jamii, mkutano ambao ulipata baraka pia kutoka
kwa Askofu mkuu Claudio Maria Celli, Rais wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano ya Jamii.
Wajumbe katika taarifa na shuhuda na majadiliano ya kina, wamekiri kwamba mitandao
ya kijamii imeleta mwelekeo mpya katika maisha ya kijamii na kiroho, mambo ambayo
yanafanyiwa kazi na Mama Kanisa kwa wakati, ili kutoa majiundo makini yatakayosaidia
watu kuwa na matumizi bora na sahihi ya mitandao ya kijamii.
Wajumbe wanakiri
kwamba, vijana wa kizazi kipya ndio wanaotumia kwa wingi maendeleo ya teknolojia ya
habari, ikilinganishwa na watu wenye umri mkubwa ambao wengi wao wamebaki kidogo nyuma,
changamoto kwa Mama Kanisa kutumia fursa hii, ili vijana waweze kuwa na mahusiano
thabiti si tu katika maisha yanayoelea katika ombwe, bali kwa kujikita katika uhalisia
wa maisha!
Mitandao ya kijamii ni jukwaa la maisha na wala si tu kitendea
kazi, kumbe kuna haja ya kukazia kile kinachowekwa kwenye mtandao kiwe ni uhusiano
na maisha ya watu kama anavyokazia Baba Mtakatifu Francisko. Lengo ni kusaidia ili
kweli, watu waguswe katika undani wa maisha yao: kiakili, kiroho na kimwili, kwa kutambua
kwamba, Yesu Kristo amewaletea ukombozi na maisha mapya kwa njia ya mateso, kifo na
ufufuko wake. Kanisa halina budi kuhakikisha kwamba, ujumbe wake unawagusa watumiaji
wa mitandao ya kijamii. Kanisa katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi
na teknolojia, linaendelea kukabiliana na changamoto mbali mbali ambazo halina budi
kuzifanyia kazi, ili kuhakikisha kwamba, kweli Injili ya Furaha inawafikia Watu wa
Mataifa.
Mitandao inayomilikiwa na kusimamiwa na Kanisa imeendelea kuwa na
mvuto kwa watu wengi wanaotaka kuzima kiu yao kuhusu kweli za Kiinjili. Uwanja wa
mawasiliano ya kijamii una kero na kinzani zake kwa Kanisa na Mafundisho yake, lakini
bado Mama Kanisa anataka kuhakikisha kwamba, “anakula sahani moja” na watumiaji wa
mitandoa ya kijamii hadi kieleweke!
Makanisa mahalia yanachangamotishwa kuhakikisha
kwamba, yanajihusisha katika matumizi ya njia za mawasiliano ya kijamii, ili kutangaza
maisha na utume wa Kanisa kwa watu mahalia. Kwa Makanisa yale ambayo waamini wake
wengi ni watumiaji wazuri wa mitandao ya kijamii, wanaweza kushirikishana kwa ajili
ya ustawi na maendeleo ya Kanisa mahalia, kwa kujenga mahusiano ya karibu zaidi.
Katika
ulimwengu wa mawasiliano ya kijamii, Mama Kanisa anataka kudumisha: umoja na mshikamano
kati ya watu, ili kukoleza maboresho ya mahusiano na maisha ya kijamii yanayojikita
katika matumizi ya mitandao ya kijamii.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa
ya Kiswahili ya Radio Vatican.