Burkina Faso imefungua ukurasa mpya kwa Serikali ya kijeshi inayoongozwa na Luteni
Kanali Isaac Zida kwa kuanza na mchakato wa upatanisho wa kitaifa ili hatimaye, kurejesha
utawala wa kiraia nchini humo ifikapo mwezi Novemba 2015. Serikali ya kijeshi imetoa
pia fursa kwa viongozi wa Chama cha CDP kilichokuwa kinaongozwa na Rais Blaise Compaorè
aliyebwaga manyanga hivi karibuni, kushiriki katika mchakato wa kuunda Serikali ya
mpito.
Vyama vya kisiasa na kijamii nchini Burkina Faso vimeridhia vigezo
na sifa anazopaswa kuwa nazo mwananchi wa Burkina Faso atakepewa dhamana ya kuongoza
Serikali ya kipindi cha mpito hadi kufikia uchaguzi mkuu, hapo mwakani.
Luteni
Kanali Issac Zida ametupilia mbali vitisho vilivyotolewa na Umoja wa Afrika kwa kuitaka
Serikali ya kijeshi kuhakikisha kwamba, inarudisha madaraka mikononi mwa raia katika
kipindi cha siku kumi na tano, vinginevyo, ingekiona kile kilichomnyoa Kanga manyoya!
Luteni Kanali Zida anasema, jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, Burkina Faso inafikia
muafaka wa kitaifa, ili hatimaye, kuweza kufanikisha mchakato wa uchaguzi mkuu unaotarajiwa
kufanyika mwezi Novemba 2015 kwa kuzingatia misingi ya haki, amani na utulivu.