2014-11-10 08:09:30

Hija ya kuombea haki na amani nchini Nigeria!


Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria kuanzia tarehe 14 hadi tarehe 15 Novemba 2014 linafanya hija ya sala mjini Abuja kwa ajili ya kuombea amani, upendo na mshikamano wa kitaifa wakati huu Nigeria inapoendelea kupepetwa kama ngano kutokana na vitendo vya kigaidi vinavyofanywa na Kikundi cha kigaidi cha Boko Haram, ambacho kwa sasa ni tishio la watu na mali zao nchini Nigeria.

Askofu mkuu Ignatius Kaigama, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria anasema, hiki ni kilele cha jitihada za Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria katika mchakato wa kutafuta haki, amani na mshikamano wa kitaifa, zilizoanza hapo Juni, 2014. Katika kipindi chote hiki, Kanisa Katoliki nchini Nigeria limekuwa na nia maalum kwa kila mwezi, ili kumwomba na kumlilia Mwenyezi Mungu ili aweze kuingilia kati baada ya jitihada za kibinadamu kuonekana kana kwamba zinagonga mwamba wa matumaini.

Kimekuwa ni kipindi cha sala, tafakari pamoja na Ibada ya kuabudu Ekaristi Takatifu, kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi. Mshikamano huu wa sala utajionesha kwa namna ya pekee pia katika hija ya kitaifa inayotarajiwa kufanyika tarehe 13 Novemba 2014.

Wakati wote huu wa majaribu na mashaka makubwa, Kanisa limeendelea kushikamana na Familia ya Mungu nchini Nigeria kwa hali na mali. Itakumbukwa kwamba, Mwezi Julai, nia ya Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria, ilikuwa ni kumlilia Mwenyezi Mungu ili watu waliotekwa nyara waweze kuachiliwa huru ili kujiunga na ndugu zao tena. Mwezi Agosti, Kanisa likasali kwa ajili ya wananchi wote wa Nigeria ambao wameguswa kwa namna moja au nyingine kutokana na mashambulizi ya kigaidi yanayotokea mara kwa mara nchini humo kana kwamba, vyombo vya ulinzi na usalama vimekwenda “likizo”.

Mwezi Septemba, Familia ya Mungu nchini Nigeria imewakumbuka na kusali kwa namna ya pekee ili kuwaombea askari wa vyombo vya ulinzi na usalama waliofariki dunia huku wakitekeleza dhamana ya ulinzi na usalama kwa raia na mali zao, bila hata ya kujibakiza, kwa kuzingatia kanuni maadili na sheria za kazi, bila usaliti wowote. Ni watu ambao wamefariki dunia na wengi kujeruhiwa wakiwa katika harakati za kulinda amani.

Mwezi Oktoba, Kanisa limesali kwa ajili ya kuombea umoja, amani na utawala bora mambo ambayo kukosekana kwake kumelitumbukiza taifa katika majanga makubwa ya mauaji ya kutisha, hofu na mashaka kwa watu na mali zao. Kwa mwezi Novemba, Familia ya Mungu nchini Nigeria inasali na kumwomba Mwenyezi Mungu ili awawezeshe kuwa na ujasiri wa kupambana na wizi, rushwa na ufisadi wa mali ya umma kwa kujikita katika misingi ya haki, ukweli na uwazi.

Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria linasema kwamba, Mwezi Desemba, Kanisa litaendelea kusali kwa ajili ya kuombea tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, ili kweli waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema waweze kusimama kidete kulinda na kutetea zawadi ya maisha, tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake hadi mauti ya kawaida inapomfika kadiri ya mpango wa Mungu. Ni changamoto ya kuendelea kutangaza Injili ya Familia kwa njia ya ushuhuda makini wa maisha adili na matakatifu.

Imehaririwa na
Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.