Azimio la Arusha katika kupambana na ujangili Kusini mwa Ikweta!
Waziri mkuu wa Tanzania Mizengo Pinda amesema inahitajika dhamira ya kweli kutoka
kwa wadau wote katika kutekeleza Azimio la Arusha la kukabiliana na ujangili na kuendeleza
hifadhi za wanyama katika nchi za Afrika Mashariki na zilizo Kusini mwa Ikweta. Akizungumza
na waandishi wa habari Jumamosi, Novemba 8, 2014 mara baada ya kufunga mkutano wa
kikanda wa siku mbili uliojadili mbinu za kupambana na biashara haramu ya wanyamapori
ulioandaliwa na Wizara ya Maliasili na Utalii jijini Arusha, Waziri Mkuu alisema:
“Suala hili linataka uwajibikaji wa pamoja. Mashirika na taasisi, wananchi na viongozi
sote kama wadau wakuu, kila mmoja anapaswa kushiriki vita hii kama kweli tunataka
tuitokomeze.” “Kwenye hili Azimio la Arusha na nyie waaandishi wa habari pia mna
sehemu yenu mmetajwa... wamesema wanatafuta jinsi ya kushirikiana na vyombo vya habari
ili visaidie kutoa elimu kwa jamii kama njia ya kuelimisha umma,” alisema. Waziri
Mkuu aliwaeleza waandishi hao kwamba Azimio hilo lina vipengele 20 ambavyo vinataka
utekelezaji katika ngazi ya nchi mojamoja, ngazi ya kanda na ngazi ya kimataifa kwa
kushirikiana na wadau wa maendeleo. “Nimepata faraja kwamba mkutano huu haukuisha
kijumlajumla tu, bali umekuja na maazimio 20 ambayo yametengwa kwa ajili yetu sisi
wa ndani, mengine yanahusisha ushirikiano wa kikanda na yako mengine yanawahusisha
wadau wa maendeleo,” alifafanua. Ili kutekeleza azimio hili, nimeshauri iundwe
timu itakayoshirikisha vyombo vingi zaidi badala ya kuiachia Wizara ya Maliasili na
Utalii peke yake. Timu hii ikutane kila baada ya miezi sita ili kufuatilia utekelezaji
wa maazimio haya na ikibidi Waziri atoe taarifa bungeni kuhusu utekelezaji huo,” alisema
Waziri Mkuu. Mapema, akizungumza na washiriki wa mkutano huo wakati wa kuufunga,
Waziri Mkuu alisema kuwepo kwa watu wa ngazi tofauti kwenye mkutano huo ni kielelezo
tosha cha umakini wao na nia thabiti ya kutokomeza ujangili katika ukanda huu. “Tumeanzisha
vita, tusisahau kwamba bado kuna kazi kubwa mbele yetu na vita haijaisha. Tuzidishe
mapambano katika sehemu tatu: kwenye nchi unakofanyika ujangili, nchi ambazo nyara
zinapitishwa na nchi zinazopokea ama kununua hizo nyara,” alisema Waziri Mkuu. “Nakubaliana
nanyi kwamba hakuna nchi inayoweza kukabili suala la ujangili ikiwa peke yake. Tunahitaji
tuwe na sera mahsusi, sera ya pamoja ya kutuunganisha na kutuongoza wakati tukitekeleza
Azimio hili kwa kusaidiana na wadau wa maendeleo,” alisema. Alisema Azimio hilo
litaipa kazi ya ziada ya Wizara ya Maliasili na Utalii ambapo kazi kubwa itakuwa ni
kusimamia na kuhakikisha utekelezaji wa wa Azimio hilo unakuwa wa ufanisi. Jumla ya
nchi tisa zimetia saini azimio hilo mbele ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda. Nchi hizo
ni Burundi, Kenya, Uganda, Msumbiji, Tanzania, Sudan Kusini, Zambia, Rwanda na Malawi.