2014-11-08 08:35:02

Sakata la magendo ya pembe za ndovu kati ya China na Tanzania!


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa nchini Tanzania Bwana BERNAD MEMBE ameutaarifu umma wa watanzania na dunia kwa ujumla kwamba madai yaliyotolewa na taasisi isiyo ya kiserikali ya London Environmental investigation Agency EIA hayana ukweli wowote.

Pia amekanusha madai ya kwamba serikali ya Tanzania haijali na wala haichukui hatua dhidi ya wanaojishughulisha na biashara haramu ya pembe za ndovu. Akitoa tamko la serikali kuhusiana na shutuma iliyotolewa na taasisi hiyo dhidi ya serikali ya Tanzania Bungeni mjini Dodoma, MEMBE amesema taarifa hizo zote ni za kupikwa na kuungwa mkono ili kuchafua heshima ya Tanzania na heshima ya Taifa la China.

Ametaja sababu za kusema taarifa hizo ni za uongo kuwa taarifa kama hiyo sio mara ya kwanza kutolewa iliwahi kutolewa mwaka 2013 na mtoa taarifa ambaye ametajwa kuwa chanzo cha habari ni mtu mmoja ambaye walimkuta barabarani na kuanza kumuuliza maswali hali sio mtumishi wa bandari wala uwanja wa ndege.

Mbali na hilo amesema ziara ya rais huyo wa China ilikuwa ya masaa 24 na programu yake ilianza mara tu alipowasili nchini kuanzia saa 9 alasiri hadi saa 4 usiku kwenye dhifa ya Taifa na kuhoji hizo shopping zinazoelezwa kufanywa na ujumbe wa rais huyo zilifanywa muda gani.

Mheshimiwa MEMBE amewataka watanzania kutokubali upuuzi wa aina hiyo kwa kuwa Tanzania ni Taifa huru halichaguliwi marafiki wala halirithishwi maadui na kuahidi kuendeleza ushirikiano uliopo wa kidugu na China na kwame hawarudi nyuma kutokana na maneno ya uwongo na uzushi.

Vyombo vya habari vya ndani na nje ya nchi vilitoa habari kwamba ujumbe wa rais wa China uliokuja nchini Tanzania miezi 18 iliyopita ulijihusisha na ununuzi wa pembe za ndovu nchini Tanzania na chanzo cha habari kikiwa ni kutoka kwa Taasisi hiyo ya EIA.

Wakati huo huo Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wameridhia azimio la kumpongeza spika wa bunge hilo mheshimiwa ANNE MAKINDA kwa kuchaguliwa kuwa rais wa Jukwaa la Mabunge ya Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC-PF).

Akisoma azimio hilo bungeni mjini Dodoma Mwenyekiti wa kamati ya mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa mheshimiwa MUSSA ZUNGU amemzungumzia mheshimiwa MAKINDA kuwa ni mzoefu wa kutosha katika medani za siasa na uongozi kwa zaidi ya miaka 37 kwa kushika nyadhifa mbalimbali kitaifa na kimataifa.

Amesema kutokana na jitihada mbalimbali zinazofanywa na rais JAKAYA KIKWETE za kuitangaza nchi ya Tanzania zilisaidia sana katika mchakato wa kumnadi mheshimiwa MAKINDA kwa wajumbe wa mkutano na kufanikiwa kushinda kwa kishindo bila ya kupingwa.

Wakiunga mkono azimio hilo baadhi ya wabunge waliochangia wamempongeza mheshimiwa MAKINDA na kusema ni mtu anayestahili kupata nafasi hiyo kutokana na uchapakazi wake.

Mbunge wa Kigoma Kaskazini mheshimiwa ZITTO KABWE amesema kwa mara nyingine tena Tanzania imeshamiri katika medani ya dunia kitu ambacho kinaleta heshima kubwa na ni ishara ya mafanikio makubwa ya kidiplomasia katika nyanja ya kimataifa.

Amesema kupata kwake nafasi hiyo kunaonyesha wazi kuwa ni jinsi gani bunge la Jamhuri lilivyokuwa halikufanya makosa kumchagua kuwa spika na kusema ana aamini atapeperusha bendera ya Tanzania vizuri anakokwenda na kuwataka wabunge kumuunga mkono kwa kuwa ni mtu mzuri.

Kwa upande wake mbunge wa viti maalum mheshimiwa BERNADETA MUSHASHU ameungana na wengine kumpongeza na kusema hawakukosea kumchagua kwa kuwa sifa anazo kutokana na kuandaliwa na Taifa hili na kumuomba mungu ampe uwezo mkubwa wa kupeperusha bendera ya Tanzania.

Mbunge wa viti maalum mheshimiwa RUKIA AHMED amesema anaona fahari kutokana na ushindi huo na kwamba uteuzi huu haujaja bure bali umekuja kutokana na juhudi kubwa alizonazo katika utendaji kazi wake wa kutobagua dini,kabila wala vyama vya siasa.

Wakati huo huo mheshimiwa MAKINDA amewataka wabunge wa vyama vyote vya siasa kuamka na kubadilisha fikra zao ili wafikirie Maendeleo.

Mheshimiwa MAKINDA akitoa shukrani kwa wabunge amesema Maendeleo sio Taifa bali yanapaswa kuanzia kwa wabunge wenyewe kwa kuwa hivi sasa nchi nyingi duniani wanachosimamia ni suala la uchumi na upo uwezekano wa Tanzania kama wasiposimamia msingi huo ikabaki nyuma.

Amewataka kuamka na kusimamia suala hilo ingawa mwaka huu ni mgumu kwa sababu wanaelekea kwenye uchaguzi lakini isiwe sababu ya kuacha kufanya kazi na kuanza kupigana vijembe.








All the contents on this site are copyrighted ©.