Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha Miaka 25 tangu Ukuta wa Berlin ulipoanguka kwa kishindo
kikubwa bila hata watu kumwaga damu! Mabadiliko haya makubwa katika historia ya Bara
la Ulaya ni sehemu ya mchango uliotolewa kwa namna ya pekee na Rais wa Urussi wakati
huo Mikhail Gorbaciov na kwa upande mwingine, Papa Yohane Paulo II, aliyewataka watu
kutoogopa!
Ukuta wa Berlin ni kielelezo cha ukomunisti uliowagawa wananchi
wa Bara la Ulaya, kiasi hata cha kuchukiana na kudhaniana vibaya. Hiki kikawa ni kikwazo
cha mchakato wa maendeleo endelevu, kiroho na kimwili, mkwamo wa mchakato wa maendeleo
ya kiuchumi na kisiasa. Ukuta wa Berlin ni kielelezo pia cha vita baridi iliyojitokeza
mara tu baada ya Vita kuu ya Pili ya Dunia, ulimwengu ukagawanyika katika makundi
mawilina hapo pia ukawa ni mwanzo wa kuibuka kwa Umoja wa Nchi zisizofungamana na
upande wowote.
Ukuta wa Berlin ulikandamiza tunu msingi za maisha ya binadamu;
ukawa ni kikwazo kikuu cha demokrasia na mzunguko wa watu na mawazo; haki msingi za
binadamu, utu na heshima ya binadamu vikawekwa rehani na hapo mashindano ya silaha,
ili kupimana nguvu yakazuka kwa kasi ya ajabu. Katika kipindi hiki kigumu katika historia
ya maisha ya wananchi wa Bara la Ulaya, Vatican na Ufaransa zilizchangia kwa kiasi
kikubwa katika majadiliano ya kidiplomasia, kwa kuhamasisha umuhimu wa kusimama kidete
kutetea na kudumisha uhuru, haki msingi za binadamu na umoja na mshikamano kati ya
watu.
Kunako mwaka 1978, Karol Wojtyla, akachaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki,
kiongozi aliyeonja adha ya Pazia la Chuma, huu ukawa ni mwanzo wa cheche za mapinduzi
Ulaya ya Mashariki, kwa kukazia mshikamano kati ya watu. Papa Yohane Paulo II akakazia
kwa namna ya pekee majadiliano na ushirikiano kati ya Serikali na Kanisa wakati alipofanya
hija yake ya kwanza ya kichungaji nchini Poland kunako mwaka 1979. Alitambua mapungufu
yaliyokuwa yamejitokeza katika mfumo wa Kikomunisti, kwa kuwa na mwono tenge kuhusu
mwanadamu pamoja na kujenga jamii inayoelea kwenye ombwe!
Dr. Joaquin Navarro-Valls,
Msemaji mkuu wa Vatican kwa wakati huo, anafafanua kwamba, Rais Mikhail Gorbaciov
alikiri mwenyewe kwamba, bila uwepo na mchango wa Papa Yohane Paulo II, kuanguka kwa
Ukuta wa Berlin ingelikuwa ni ndoto ya mchana! Rais Gorbacion alisoma kwa makini mchango
wa Baba Mtakatifu Yohane Paulo II katika Mafundisho Jamii ya Kanisa, akajichotea utajiri
mkubwa, uliomsaidia kuwa na mwelekeo mpya katika kuharakisha mapinduzi ya kisiasa
nchini mwake. Papa Yohane Paulo II alikazia pamoja na mambo mengine, uhuru na ukweli;
demokrasia, utu na heshima ya binadamu.
Ilikuwa ni tarehe 9 Novemba 1989 umati
wa watu kutoka Ujerumani ya Mashariki ulipovuka ukuta, huku bunduki zikiwa zimeinamishwa
chini, Urussi ikashindwa kuingilia masuala ya ndani ya Ujerumani na Askari wakapewa
amri ya kubaki majumbani mwao. Viongozi wakuu wa nchi mbali mbali wakapigwa butwaa,
huo ukawa ni mwanzo wa ukurasa mpya wa historia ya Bara la Ulaya. Ujerumani ikaungana
tena na nchi nyingi zilizokuwa chini ya utawala wa Kisovieti zikaanza kuporomoka kama
matofali ya kuchoma".
Tarehe Mosi, Desemba 1989 Rais Mikhael Gorbaciov akakutana
na Mtakatifu Yohane Paulo II mjini Vatican; mipaka ya Ujerumani ikachorwa upya, vita
baridi, vikahifadhiwa kwenye kumbu kumbu za kihistoria na Ukomonisti, ukapelekwa kwenye
chumba cha wagonjwa mahututi ie. ICU!
Imehaririwa na Padre Richard A. Mjigwa,
C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.