Wakristo na Wasikhi wanahamaishwa kudumisha huduma ya upendo!
Baraza la Kipapa la majadiliano ya kidini limewaandikia waamini wa dini ya Kisikh
ujumbe wa amani, matashi mema na mshikamano wa kidugu katika maadhimisho ya Siku kuu
ya Guru Nanak Jayanti, iliyoadhimiwa, hapo tarehe 6 Novemba 2014 kwa kuongozwa na
kauli mbiu "Wakristo na Wasikhi: kwa pamoja dumisheni huduma ya upendo".
Sherehe
hizi zisaidie kujenga na kudumisha mshikamano, utulivu na amani, wakati wanapotoa
huduma katika Jamii. Kwa Wakristo, Yesu Kristo ni kielelezo cha matendo ya huruma
kama inavyojionesha katika Maandiko Mtakatifu, kwa kujifananisha na Msamaria mwema.
Kwa Wasikhi, upendo na huduma ni mambo yanayopewa kipaumbele cha kwanza katika maisha
yao, kwa kutoa kipaumbele cha pekee kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa
Jamii, wagonjwa, wazee, wahamiaji, wakimbizi, wanaodhulumiwa na kunyanyaswa, kwa kutambua
kwamba, binadamu wote ni kazi ya Mwenyezi Mungu.
Upendo na majitoleo binafsi
katika huduma ni mambo muhimu sana katika kukuza upendo na mshikamano na wengine.
Kila mtu anapaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa utu na heshima yake kwani ana thamani
ya pekee mbele ya Mwenyezi Mungu kama anavyosema Baba Mtakatifu Francisko.