2014-11-07 14:56:26

Shikamaneni kidugu katika Kristo ili kukabiliana na changamoto mamboleo!


Fumbo la Ekaristi Takatifu ni kielelezo cha umoja na mshikamano kati ya watu wa Mungu na matunda yake ni kupenda kusoma na kulitafakari Neno la Mungu, ili kuishi kadiri ya matakwa ya Injili pamoja na kuendeleza upendo, urafiki, udugu na mshikamano kati ya watu, tayari kusoma alama za nyakati, huku waamini wakimsikiliza Roho Mtakatifu kwa unyenyekevu.

Huu ndio ushuhuda unaojikita katika udugu unaofumbatwa katika maisha ya Kikristo, alama wazi yenye mvuto na mguso katika imani kwa Kristo Mfufuka. Ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 7 Novemba 2014 alipokutana na kuzungumza na wajumbe wa Chama cha Fokolare, waliomtembelea mjini Vatican kwa kukazia kwamba, Wakristo wanapaswa kuungana na kutekeleza changamoto mbali mbali zinazojitokeza katika uso wa dunia kwa njia ya mshikamano wa kidugu.

Kwa njia hii wataonesha kwa imani katika matendo utandawazi wa mshikamano na udugu miongoni mwa Wakristo. Katika nchi nyingi bado kunakosekana uhuru wa kuabudu na kuishi kiaminifu kadiri ya kanuni maadili ya Kikristo; kuna Wakristo wanaoendelea kunyanyaswa na kudhulumiwa kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake; vitendo vya kigaidi vinazidi kushika kasi ya ajabu; bado kuna mateso na mahangaiko kwa wakimbizi na wahamiaji; misimamo mikali ya kiimani; tatizo la watu kukumbatia malimwengu; mambo ambayo yanapaswa kupewa uzito wa pekee katika dhamiri kama Wakristo na Viongozi wa Kanisa.

Katika changamoto za namna hii anasema Baba Mtakatifu, kuna haja ya kutafuta njia mpya na endelevu zinazosimikwa katika uvumilivu, ili kufikia umoja na hatimaye, kuwawezesha watu kuamini, kwa kuonesha imani na ujasiri unaofumbatwa katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, kielelezo cha umoja na mshikamano.

Mtakatifu Paulo anaonesha kwa namna ya pekee kwamba, Ekaristi Takatifu ni kiini cha maisha ya Kikristo, wakati wa ukweli na fursa ya kukutana na neema kutoka kwa Yesu kwa njia ya uwajibikaji. Kwa njia ya Fumbo la Ekaristi, waamini wanatambua kwamba, umoja ni zawadi inayowawajibisha. Baba Mtakatifu Francisko amewatakia wajumbe wa Chama cha Kitume cha Wafokolari kuzaa matunda ya ukomavu katika kudumisha umoja, huku wakishuhudia udugu.







All the contents on this site are copyrighted ©.