2014-11-07 12:04:19

Msalaba wa Kristo unafumbata: Unyenyekevu, ufukara, upole, huduma, ibada na sala!


Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake Ijumaa tarehe 7 Novemba 2014 kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican amewaonya kwamba, hata leo hii kuna Wakristo ambao ni maadui wa Msalaba wa Kristo, lakini bado wanashiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa, huku wakiwa wamekumbatia malimwengu, kwa jina ni Wakristo, lakini matendo yao ni ya kipagani kabisa!

Kutokana na maisha kama haya, Wakristo wa namna hii ni hatari kwa ustawi na maendeleo ya Kanisa la Kristo, kwani ni watu wa majina, lakini maisha yao ni kinyume kabisa cha imani wanayoiungama, ni watu wanaotafuta mambo ya kidunia na kusahau kwamba, hapa duniani ni wasafiri na wala hawana makazi ya kudumu. Ni watu wenye uchu wa mali na madaraka; watu wanaopenda kujikweza na kujivuna mbele ya watu badala ya kujinyenyekeza, kumpenda Mungu na jirani, ili kuanza kujiandalia makazi ya mbinguni kwenye maisha ya uzima wa milele.

Baba Mtakatifu akizungumzia Injili ya siku amesikitishwa na maovu yaliyotendwa na yule Wakili mwenye busara ambaye alitenda kazi zake kwa mazoea ya kuiba kidogo kidogo na hatimaye akajikuta amekuwa ni fisadi wa kutupwa, hawa ndio adui wa Msalaba wanaozungumziwa na Mtakatifu Paul.

Hii ni changamoto na mwaliko kwa Wakristo kushikamana na Kristo na kamwe wasikubali kishawishi cha kuwa ni wapinga Msalaba wa Kristo, bali watu wenye matumaini ya wokovu, ambao miili yao ya uharibifu itabadilishwa kuwa ni miili ya utukufu. Msalaba wa Kristo unafumbata: unyenyekevu, ufukara, upole, huduma, ibada na sala!







All the contents on this site are copyrighted ©.