Komesheni mauaji ya watu wasiokuwa na hatia huko Mashariki ya Kati!
Askofu mkuu Bernadito Auza, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Umoja wa Mataifa,
hivi karibuni akishiriki katika mkutano wa 69 wa Baraza kuu la Umoja wa Mataifa ametumia
fursa hii kutoa salam zake za rambi rambi kwa familia za wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa
waliouwawa kikatili wakati wakitoa msaada kwa wakimbizi wa Palestina.
Hadi
sasa inaonekana kwamba, mchakato wa amani katika Ukanda wa Ghaza bado unechechemea
na matokeo yake watu wanaendelea kupoteza maisha pamoja na uharibifu wa miundo mbinu.
Vatican inapenda kuiomba Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inakomesha mauaji
ya watu wasiokuwa na hatia; kwa kudhibiti biashara haramu ya silaha huko Mashariki
ya Kati ili fedha hiyo iweze kutumika kuchochea huduma na maendeleo ya watu.
Vatican
inapenda kuonesha mshikamano wake na Wakristo wanalazimika kuyakimbia makazi yao huko
Mashariki ya Kati kutokana na nyanyaso na dhulumu za kidini na kwamba, Kanisa Katoliki
kwa kushirikiana na wadau mbali mbali, litaendelea kutoa huduma ya elimu, afya na
maendeleo kwa wananchi wengi wanaoishi vijijini bila ubaguzi, mwaliko kwa Jumuiya
ya Kimataifa kuendelea kuonesha mshikamano wa upendo na udugu kwa wananchi wanaoishi
huko Mashariki ya Kati.
Askofu mkuu Auza anasema kwamba, Jumuiya ya Kimataifa
inashiriki katika mchakato wa upatikanaji wa amani huko Mashariki, lakini Israeli
na Palestina wanapaswa kutambua kwamba, wao ndio wadau wakuu, wanaopaswa kuheshimiana
na kuthaminiana; kwa kujenga na kudumisha uhuru wa kidini ili kweli amani iweze kutawala
katika mioyo ya watu.