Changamoto katika mapambano dhidi ya uhalifu wa kimataifa!
Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha kumbu kumbu ya miaka 100 tangu Jeshi la Polisi Kimataifa,
Interpol lilipoanzishwa, mwaliko kwa vikosi vya ulinzi na usalama kushirikiana kwa
karibu zaidi katika kupambana na changamoto za ulinzi na usalama kwa nyakati hizi.
Uwepo wa Interpol umesaidia kuimarisha ulinzi na usalama kwa familia ya binadamu
na kwamba, Vatican itaendelea kushirikiana na Jumuiya ya Kimataifa ili kuenzi juhudi,
kwa kukazia utawala wa sheria, haki, amani, utu na heshima ya binadamu.
Huu
ni mchango uliotolewa na Askofu mkuu Dominique Mamberti, Katibu mkuu wa mambo ya nchi
za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican wakati wa mkutano wa themanini na
tatu wa Interpol, ulioanza hapo tarehe 3 hadi tarehe 7 Novemba 2014, huko Monaco.
Anasema, Baba Mtakatifu Francisko katika utume wake, anaendelea kuwahimiza watu wa
mataifa kujenga na kudumisha utamaduni wa kukutana unaopania kuimarisha mahusiano
ya kijamii, utu, heshima ya binadamu na mshikamano kati ya watu.
Katika ulimwengu
wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia, uhalifu wa kimataifa umeongezeka
maradufu, kutokana na: mwingiliano wa watu, wepesi wa kusafrisha fedha na bidhaa na
matokeo yake ni kama vita inayoendelea huko Mashariki ya Kati. Uhalifu wa kimataifa
unatumia silaha kali na zinazosababisha uhalibifu mkubwa. Jumuiya ya Kimataifa inakabiliana
pia na biashara haramu ya binadamu inayojionesha katika sura mbali mbali mambo ambayo
kamwe hayawezi kukubalika.
Askofu mkuu Mamberti anasema, Vatican itaendelea
kushirikiana na Jumuiya ya Kimataifa katika malezi ya dhamiri nyofu, kwa kukazia haki
msingi za binadamu, utu na heshima yake; uhuru na wajibu wa Serikali husika katika
kudumisha utawala wa sheria. Pengo kubwa la maendeleo kati ya watu ni chanzo kikubwa
kinachosababisha mipasuko ya kijamii na matokeo yake ni kinzani na vita; mambo ambayo
pia yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na mtikisiko wa uchumi kimataifa. Maendeleo ya
sayansi ya mawasiliano ya jamii yamekuwa pia ni tishio kwa amani na usalama wa Jumuiya
ya Kimataifa.
Askofu mkuu Mamberti anasema kuna haja ya kukuza na kudumisha
utawala wa sheria, mahusiano bora ya kijamii kwa kuzingatia tamko la Umoja wa Mataifa
kuhusu haki msingi za binadamu; utu na heshima ya binadamu pamoja na kusimama kidete
kulinda na kutetea mafao ya wengi. Ikumbukwe kwamba, binadamu ana haki na wajibu anaopaswa
kutekeleza hata pale anapopatikana na hatia ya kuvunja sheria. Adhabu ilenge kuleta
maboresho katika maisha ya mhusika ili anapohitimisha adhabu yake aweze kurejea tena
katika Jamii na kuendelea na maisha kama kawaida.
Askofu mkuu Dominique Mamberti
anaitaka Jumuiya ya Kimataifa kutumia rasilimali watu na fedha kwa ajili ya maendeleo
ya watu: kimaadili, kitamaduni na kiuchumi, kwani maendeleo na mshikamano wa kimataifa
ni jina jipya la amani ya kudumu. Serikali pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama
vikifanikiwa kutekeleza dhamana na wajibu wake katika mazingira kama haya, hapo Jamii
inaweza kupambana fika na uhalifu.
Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuendelea
kuwekeza katika mapambano dhidi ya: uhalifu na ufadhili dhidi ya vitendo vya kigaidi;
ugaidi wa kibailojia, utakatishaji wa fedha haramu, biashara haramu ya silaha ambayo
ni chanzo kikuu cha majanga ya kitaifa na kimataifa pamoja na biashara haramu ya binadamu,
inayodhalilisha utu na heshima ya binadamu.
Vatican katika siku za hivi karibuni
imeweka sheria na mikakati ya kupambana kikamilifu na vitendo hivi na kwamba, itaendelea
kushirikiana na Jumuiya ya Kimataifa, ili kufanikisha malengo haya!
Imehaririwa
na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.