2014-11-07 07:40:33

Burkina Faso kufanya uchaguzi mkuu Novemba 2015


Baraza la Maaskofu Katoliki Burkina Faso linapongeza hatua ambayo imefikiwa na Serikali ya mpito inayoongozwa na Jeshi baada ya majadiliano ya kina na viongozi wa Jumuiya ya Kiuchumi, Afrika Magharibi, yaani ECOWAS, itakayoiwezesha Burkina Faso kufanya uchaguzi mkuu hapo Novemba 2015, mwaka mmoja kuanzia sasa. Katika makubaliano hayo, Serikali ya Kijeshi, itabidi kuachia madaraka kwa utawala wa kidemokrasia ifikapo mwaka 2015 na kwamba, uchaguzi mkuu utasimamiwa na Rais wa kipindi cha mpito, ambaye anatarajiwa kuteuliwa hivi karibuni.

Baraza la Maaskofu Katoliki Burkina Faso katika ujumbe wake kwa waamini na wananchi wenye mapenzi mema nchini humo wanawataka wanasiasa kwa namna ya pekee kabisa kuhakikisha kwamba, kulinda na kutetea mafao ya wengi, kwa kuzingatia matarajio ya wananchi wa Burkina Faso pamoja na Jumuiya ya Kimataifa.

Maaskofu wanashauri kwamba, ikiwezekana viongozi wa Serikali ya mpito wasishiriki katika uchaguzi mkuu utakaofanyika mwezi Novemba 2015. Kipindi hiki cha mpito, iwe ni fursa ya kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu, kwa kulinda na kudumisha amani, utulivu na mshikamano wa kitaifa. Maaskofu wanawapongeza wananchi wa Burkina Faso walionesha nguvu ya umma ili kuleta mabadiliko katika nchi yao kwa kukazia utawala wa sheria unaozingatia Katiba ambayo kimsingi ni sheria mama!







All the contents on this site are copyrighted ©.