2014-11-06 07:48:51

Ujumbe wa amani na matumaini kwa wananchi wa Burkina Faso!


Baraza la Maaskofu Katoliki Burkina Faso katika mkutano wake wa siku mbili uliohitimishwa hivi karibuni, limetoa ujumbe wa amani na matumaini kwa wananchi wa Burkina Faso, kwa kuwataka kuwa kweli ni wajenzi na vyombo vya haki, amani na upatanisho.

Kanisa linatambua dhamana na wajibu wake wa kuwa ni vyombo vya huduma ya haki, amani na upatanisho na kwamba, kama Kanisa, waliwahi kuonya kwamba, vijana wengi nchini Burkina Faso walikuwa wamekata tamaa na kuchangayikiwa na kwamba, hali hii ilipaswa kurekebishwa mapema kabla ya madhara makubwa hayajatokea! Lakini Waswahili wanasema, usipoziba ufa utajenga ukuta!

Maaskofu wanakumbusha kwamba, Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI alipotembelea nchini Benin kunako mwaka 2011 ili kuzindua matunda ya Awamu ya Pili ya Sinodi maalum ya Afrika, akizungumza na viongozi wa kisiasa na wachumi kutoka Barani Afrika, aliwataka kutowapokonya watu wao matumaini ya kesho iliyo bora zaidi, kwa kuwawekea giza, bali wahakikishe kwamba,wanawajibika kimaadili na daima wakijitahidi kutafuta hekima ya Kimungu, ili waweze kufahamu mapenzi ya Mungu kwa ajili ya watu wao, ili hatimaye, waweze kuwa ni vyombo vya matumaini.

Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, aliwaambia viongozi wa Bara la Afrika kwamba, si rahisi kuhimili kishindo cha vishawishi na majaribu katika ulimwengu mamboleo kwa kutambua kwamba, uongozi ni huduma kutokana na uchu wa mali na madaraka mambo ambayo yanawatumbukiza viongozi wengi kushindwa kusimama kidete kulinda na kutetea mafao ya wengi na matokeo yake kuendekeza: ubinafsi, ukabila na udini. Ni Mungu mwenyewe anayeweza kuwakirimia waja wake nia njema.

Baraza la Maaskofu Katoliki Burkina Faso linapenda kuungana na wale wote waliopoteza ndugu zao wakati wa machafuko na maandamano yaliyopelekea Serikali iliyokuwa madarakani "kubwaga manyanga". Wanapongeza juhudi za uzalendo zinazooneshwa na wananchi kwa kusema kwamba, sasa ni wakati wa kufutilia mbali maovu kutoka katika undani wa mioyo yao na katika miundo mbinu ya kijamii; kulinda maisha na mali ya watu.

Maaskofu wanawaalika waamini na wananchi wa Burkina Faso katika ujumla wao, kuanza kujikita katika mchakato wa uponyaji wa ndani kwa kuwashughulikia wale walioguswa kwa namna ya pekee na machafuko ya kisiasa nchini humo, ili kudumisha ulinzi na usalama wa watu na mali zao; changamoto ya kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu.

Maaskofu katika barua yao ya kichungaji wanawataka wananchi wa Burkina Faso kuzingatia na kuheshimu utawala wa sheria na vyombo vya ulinzi na usalama; waandishi wa habari watekeleze wajibu wao kwa kuzingatia kanuni maadili, uzalendo na mustakabali wa taifa lao. Viongozi mbali mbali nchini humo waunganishe nguvu zao ili kujenga na kuimarisha umoja na mshikamano wa kitaifa, kwa ajili ya Bukrina Faso mpya.

Imehaririwa na
Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.