Ujenzi wa maghala makubwa ya kuhifadhia chakula kuanza Mwaka 2015
Waziri mkuu wa Tanzania Mizengo Pinda amekagua maghala ya kuhifadhia chakula yaliyopo
Kizota nje kidogo ya mji wa Dodoma ikiwa ni utekelezaji wa ahadi aliyoitoa Alhamisi
iliyopita kwamba Serikali inalenga kujenga maghala kwenye mikoa sita kupitia mkopo
ambao itaupata kutoka Serikali ya Poland.
Akizungumza na viongozi wa mkoa wa
Dodoma pamoja na Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) Alhamisi, Novemba 6,
2014 wakati akikagua maghala hayo, Waziri Mkuu alisema katika mkoa huo, Serikali ina
nia ya kujenga maghala makubwa (SILOS) yenye uwezo wa kuhifadhi tani 100,000 za nafaka
kwa wakati mmoja.
“Tukipata maghala yenye uwezo wa kuhifadhi tani 100,000 tutakuwa
na uhakika wa kuchukua na akiba ya nafaka kutoka mikoa ya jirani ya Singida, Tabora
na Manyara,” alisema. Waziri Mkuu alifuatana na Bw. WITOLD KARCZEWSKI ambaye ni mmiliki
wa kiwanda kikubwa cha kusindika nafaka nchini Poland ambacho Waziri Mkuu Pinda alikitembelea
alipozuru nchi hiyo Oktoba 24, mwaka huu. Bw. KARCZEWSKI anamiliki pia kiwanda kinachotengeneza
malighafi za kujengea SILOS.
Akitoa taarifa mbele ya Waziri Mkuu, Mkuu wa kituo
cha NFRA Kanda ya Kati, Bw. Ruwaichi Mambali alisema kituo hicho kina maghala yenye
uwezo wa kuhifadhi tani 30,000 lakini kwa sasa kina tani 69,000 ambazo kati ya hizo
tani 62,000 zipo Kizota (Dodoma) na tani 7,000 ziko Manyoni (Singida). Alisema eneo
zima la Kizota lina ukubwa ekari 33 na kwamba kuna maghala matatu yenye uwezo wa kuhifadhi
tani 10,000 kila moja. “Lakini kwa sasa tumelazimika kuweka mahindi mengine na mtama
hapa nje ambayo tumeyafunika kwa maturubali,” alisema.
Kwa upande wake,
Bw. KARCZEWSKI alitaka kufahamu miundombinu iliyopo kwenye ghala la Kiszota ikiwemo
umabli wa kutoka barabara kuu pamoja na reli. Pia alitaka kujua eneo zima lina ukubwa
kiasi gani. Na alitaka kufahamu mbinu zinazotumika hivi sasa kuhifadhi chakula kwenye
ghala hilo. Alisema wakipata michoro ya eneo hilo (site map), atatuma wataalamu wake
Januari mwakani waangalie uwezekano wa kuanza ujenzi mapema iwezekanavyo pindi mazungumzo
yakikamilika.
Hivi karibuni, wakati akizungumza na waandishi wa habari
jijini Dar es Salaam mara baada ya kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Mwl. Julius
Nyerere akitokea Oman, Waziri Mkuu alisema alikwenda Poland kutafuta msaada wa mfumo
wa mkopo wenye masharti nafuu ambao utasaidia kupambana na tatizo la uhaba wa maghala
kwa ajili ya kuhifadhia nafaka.
Alisema Serikali imelenga mikoa sita ya
kuanzia ambayo ni Ruvuma, Rukwa, Njombe (pamoja na Iringa) ambako kuna uzalishaji
mkubwa wa mahindi. Pia inaangalia Kanda ya Ziwa ambako mara nyingi wana uhaba wa chakula;
na kwamba itaweka maghala mkoani Dodoma kwa sababu ni katikati ya nchi ili ikusanye
akiba kutoka mikoa ya jirani ya Singida, Manyara na Tabora.
“Lengo ni
kupata uwezo wa kuhifadhi tani 700,000 hadi 1,000,000 na ujenzi wao siyo kama huu
wa kwetu. Tumewaomba watujengee SILOS (maghala makubwa) kwa sababu zina teknolojia
ya kujua kiasi gani cha nafaka kimeingia, zina unyevu kiasi gani, unaweza kuweka dawa
nafaka zako, kuosha na kukausha na kisha ukasindika kwa kiwango unachotaka,” Waziri
Mkuu aliwaeleza waandishi wa habari.
Alisema uzalishaji mwaka huu umetoa
ziada ya tani milioni 1.5 za nafaka na tani 800,000 za mpunga ikilinganishwa na ziada
ya tani 300,000 iliyokuwepo mwaka jana.“Serikali inakabiliwa na changamoto ya kupata
soko la uhakika kwa mazao ya wakulima kwa sababu tulizoea kumtumia Wakala wa Hifadhi
ya Taifa ya Chakula (NFRA) kama mnununzi mkuu na uwezo wezo wake ni tani 240,000 tu
kwa mwaka,”alisema.