2014-11-06 08:38:55

Papa Francisko kutembelea Torino, 21 Juni 2015 ili kutoa heshima kwa Sanda Takatifu!


Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake mjini Vatican, Jumatano tarehe 5 Novemba 2014 ametangaza kwamba, tarehe 21 Juni 2015 anatarajia kutembelea Jimbo kuu la Torino, Kaskazini mwa Italia, ili kutoa heshima zake kwa Sanda Takatifu pamoja na kushiriki na Familia ya Mungu Jimboni humo katika maadhimisho ya Jubilee ya miaka 200 tangu alipozaliwa Mtakatifu Yohane Bosco.

Akizungumza na waandishi wa Habari mjini Vatican, Askofu mkuu Cesare Nosiglia wa Jimbo kuu la Torino pamoja na ujumbe wake anasema kwamba, onesho la Sanda Takatifu litaanza hapo tarehe 19 Aprili na kufungwa rasmi tarehe 24 Juni 2015 na kwamba, uwepo wa Baba Mtakatifu Francisko utanogesha kilele cha maadhimisho ya Jubilee ya miaka 200 tangu kuzaliwa kwa Mtakatifu Yohane Bosco.

Maadhimisho haya anasema Askofu mkuu Nosiglia yanaongozwa na kauli mbiu "hakuna aliye na upendo mwingi kuliko huu" maneno kutoka katika Injili kama ilivyoandikwa na Yohane: 15: 13. Mtu kuyamimina maisha yake kwa ajili ya wengine ni kielelezo kikubwa cha upendo; ni mwaliko na changamoto kwa kila mwamini kutekeleza dhamana na wajibu wake kadiri ya wito na nafasi yake ndani ya Kanisa. Upendo wa Mungu kwa namna ya pekee unajionesha kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wa Yesu.

Tukio hili linatarajiwa kuwahusisha kwa namna ya pekee vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia kwani Mtakatifu Yohane Bosco, anafahamika na wengi kuwa ni Mtakatifu wa Vijana. Wagonjwa watakuwa na nafasi ya pekee katika maadhimisho haya, kwani watapata fursa ya kusali na kutafakari kuhusu mateso na mahangaiko ya mwanadamu. Waamini wanaotaka kujipatanisha na Mungu kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho, watapata fursa hii kwani kutakuwepo na Mapadre wa kutosha kwa ajili ya maungamo.

Itakumbukwa kwamba, kuanzia mwaka 1978 Mtakatifu Yohane Paulo II alitembelea Jimbo kuu la Torino na kusema kwamba, Sanda Takatifu inaonesha kwa namna ya pekee kabisa mateso na kifo cha Yesu Kristo. Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI alitembelea Torino kunako mwaka 2010. Askofu mkuu Cesare Nosiglia anasema kwamba, Sanda Takatifu ina umuhimu wake hasa katika maisha ya Kanisa na shughuli za kichungaji. Hakuna juhudi za pekee kwa ajili ya tafiti za kisayansi kwenye Sanda Takatifu.







All the contents on this site are copyrighted ©.