Mwongozo na sera mpya ya fedha kwa ajili ya taasisi na ofisi za Vatican
Kardinali George Pell, Mwenyekiti wa Sekretarieti ya Uchumi mjini Vatican anasema,
Sektretarieti yake imechapisha mwongozo na sera ya fedha kwa taasisi na ofisi mbali
mbali zinazoendeshwa na Vatican na kwamba, mwongozo huu utaanza kutumika tarehe Mosi,
Januari 2015. Mwongozo umepitishwa tayari na Baba Mtakatifu Francisko pamoja na Baraza
la Kipapa la Uchumi.
Lengo la Mwongozo huu anasema Kardinali Pell ni kuzisaidia
taasisi na ofisi mbali mbali za Vatican kufanya maboresho makubwa katika vigezo na
mchakato wa utekelezaji wa Bajeti kwa kuwa na kanuni za pamoja zinazozingatia viwango
cya kimataifa. Mkazo ni kuhakikisha kwamba, rasilimali fedha, watu na mali ya Kanisa
vinatumika kikamilifu kwa ajili ya huduma na utume wa Mama Kanisa Ulimwenguni.
Mwongozo
na Sera ya Fedha zitaendelea kuimarisha mchakato wa mabadiliko makubwa yanayofanywa
na Kanisa kwa wakati huu ili kuongeza tija, ubora, ufanisi, ukweli na uwazi katika
matumizi ya mali ya Kanisa. Hatima ya mwongozo huu anasema Kardinali Pell ni kuiwezesha
Vatican kutekeleza sera mpya katika masuala ya fedha na rasilimali ya Kanisa, kwa
kuwa na mwelekeo mpana zaidi.
Haya ni mabadiliko ambayo Makardinali walishauri
yafanyiwe kazi wakati wa mikutano yao elekezi kabla ya uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu
Petro. Matumizi ya fedha ya Kanisa yatakaguliwa na kuhakikiwa na taasisi ya kimataifa,
ili kudumisha dhana ya ukweli na uwazi katika matumizi ya mali ya Kanisa.