Mshikamano wa Baraza la Makanisa kwa wananchi wa Nigeria!
Dr. Olav Fykse Tveit, Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni amesikitishwa
na mashambulizi yanayofanywa na Kikundi cha Kigaidi cha Boko Haramu dhidi ya Makanisa
nchini Nigeria. Baraza la Makanisa Ulimwenguni linapenda kuonesha mshikamano wake
wa dhati kwa wananchi wote wa NIgeria walioguswa kwa namna ya pekee na mashambulizi
ya kigaidi ambayo yamekuwa ni tishio kwa maisha na usalama wa watu na mali zao.
Baraza
la Makanisa linawapongeza wale wote wanaojitahidi kuwahudumia watu walioathirika kutokana
na mashambulizi kwa kuyakimbia makazi yao ili kutafuta usalama wa maisha, hasa Kaskazini
mwa Nigeria. Hadi sasa wasichana 200 waliotekwa nyara hawajulikani mahali walipo na
inasemekana kwamba, wamekwisha wekwa unyumba na watesi wao, jambo ambalo halikubaliki
kamwe anasema Dr. Tveit.
Baraza la Makanisa Ulimwenguni linaiomba Serikali
ya Nigeria kuendelea kushughulikia tatizo la wasichana hao ili waweze kuachiliwa huru
haraka iwezekanavyo. Ni wazi kwamba, Nigeria inahitaji msaada kutoka katika Jumuiya
ya Kimataifa ili kupambana na Kikundi cha Kigaidi cha Boko Haram, kwani hatima na
Nigeria iko mashakani, watu wanaendelea kuteseka na kukata tamaa.
Baraza la
Makanisa linawaalika watu wote wenye mapenzi mema kuwasindikiza wananchi wa Nigeria
kwa sala zao katika kipindi hiki kigumu!