2014-11-06 14:17:57

Kinzani na utengano ni mambo yanayodhohofisha utangazaji wa Injili na ushuhuda wa upendo!


Neema na iwe kwenu, na amani itokayo kwa Mungu Baba na kwa Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye alijitoa nafsi yake kwa ajili ya dhambi zetu, ili atuokoe na dunia hii mbovu iliyopo sasa, kama alivyopenda Mungu, Baba yetu.

Ni maneno yanayojikita katika imani na matumaini kwa kumtangaza Yesu Kristo kuwa ni Bwana na Mkombozi; salam kutoka kwa Mtakatifu Paulo kwa Wagalatia, ambayo Baba Mtakatifu Francisko amependa kuibinafsisha na kuifanya kuwa yake, wakati alipokutana na kuzungumza na wajumbe wa Shirikisho la Makanisa ya Kiluteri Ulimwenguni, waliomtembelea mjini Vatican, Alhamisi, tarehe 6 Novemba 2014.

Baba Mtakatifu katika mazungumzo yake na wajumbe hawa amekazia kwa namna ya pekee umoja na mshikamano katika kumshuhudia Kristo kwa walimwengu, kwa kutambua kwamba, wote wanashiriki Ubatizo mmoja uliowawezesha kufa na kufufuka na Kristo na kwamba, kwa sasa wanaishi kwa nguvu ya Roho Mtakatifu. Yesu Kristo ni msingi na nguzo thabiti ya Jumuiya za Kikristo zinazopaswa kujibidisha katika utangazaji wa Injili unaojikita katika ushuhuda wa upendo kwa Mungu na jirani.

Baba Mtakatifu anasema, utengano na kinzani kati ya Wakristo ni mambo yanayodhofisha jitihada za Wakristo kumshuhudia Kristo kwa kutangaza Habari Njema ya Wokovu kwa Watu wa Mataifa. Utengano unaharibu umoja unaopata chimbuko lake katika neema ya Ubatizo. Wakristo wakifanikiwa kuponya madonda ya utengano ushuhuda wa Injili unaweza kupata ufanisi mkubwa, na hasa zaidi pale watakapofanikiwa kuadhimisha Mafumbo la Kanisa kwa kutangaza kwa pamoja Neno la Mungu na kulishuhudia kwa njia ya upendo.

Baba Mtakatifu amewapongeza wajumbe wa Shirikisho la Makanisa ya Kiluteri Ulimwenguni katika harakati na majadiliano mbali mbali ya kiekumene, ili kwa pamoja waweze kutangaza Habari Njema ya Wokovu kwa Watu wa Mataifa huku wakitolea ushuhuda wa pamoja. Kanisa halina budi kutafuta mbinu mpya za Uinjilishaji pamoja na kuendelea kujenga na kudumisha umoja miongoni mwa Wakristo, ili hatimaye, Wakristo waweze kuwa tena wamoja kama Kristo anavyolitaka Kanisa lake.







All the contents on this site are copyrighted ©.