Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amefanya
uteuzi wa wakuu wapya wanne wa Mikoa, amewahamisha wengine sita na ameamua kuwa wengine
watatu watapangiwa kazi nyingine.
Taarifa iliyotolewa mjini Dodoma, Jumatano,
Novemba 5, 2014 na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue inasema kuwa, Wakuu wapya
wa Mikoa ni Bi. Halima Omari Dendego ambaye anakuwa Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Dkt. Ibrahim
Hamisi Msengi ambaye anakuwa Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Bi. Amina Juma Masenza ambaye
anakuwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa na Bwana John Vianney Mongella ambaye anakuwa Mkuu
wa Mkoa wa Kagera.
Taarifa inasema kuwa kabla ya uteuzi wake Bi. Dendego alikuwa
Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Dkt. Msengi alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Bi. Masenza
alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Ilemela na Bwana Mongella alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Arusha.
Taarifa
hiyo inasema kuwa Wakuu hao wapya wa Mikoa wanapishwa, Alhamisi, Novemba 6, 2014 saa
saba mchana, Ikulu, Dar es Salaam. Aidha, taarifa hiyo imesema kuwa Wakuu wa Mikoa
ambao watapangiwa kazi nyingine ni Kanali (Mst) Fabian Massawe wa Kagera, Dkt. Christine
Ishengoma wa Iringa na Kanali Joseph Simbakalia wa Mtwara.
Wakuu wa Mikoa ambao
wamehamishwa vituo vya kazi ni Bwana Magesa S. Mulongo ambaye anakwenda Mkoa wa Mwanza
kutoka Arusha, Dkt. Rehema Nchimbi ambaye anakwenda Mkoa wa Njombe kutoka Dodoma,
Bwana Ludovick John Mwananzila anakwenda Tabora kutoka Lindi, Kapteni (Mst) Anseri
Msangi anayekwenda Mkoa wa Mara kutoka Njombe na Mhandisi Everist Ndikilo ambaye anakwenda
Arusha kutoka Mwanza.
Wengine waliohamishwa ni Luteni (Mst) Chiku A.S. Galawa
ambaye anakuwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma kutoka Tanga, Dkt. Rajab Rutengwe ambaye anakwenda
Mkoa wa Tanga kutoka Katavi, Bi Fatma Mwasa ambaye anakuwa Mkuu wa Mkoa wa Geita kutoka
Tabora na Bwana Magalula S. Magalula ambaye anahamishiwa Lindi kutoka Geita.
Taarifa
hiyo imesema kuwa Wakuu wa Mikoa ya Dar es Salaam, Kigoma, Kilimanjaro, Manyara, Mbeya,Morogoro,
Pwani, Rukwa, Shinyanga, Ruvuma, Singida na Simiyu watabakia kwenye vituo vyao vya
sasa. Aidha, Rais Kikwete amefanya uteuzi wa Wakuu wapya wa Wilaya, kuhamisha baadhi
yao na kutengua uteuzi wa baadhi. Taarifa kamili itatolewa na Waziri Mkuu baada ya
kuwa wamepangiwa vituo vya kazi.