2014-11-06 14:25:41

Jielekezeni zaidi katika ustawi na maendeleo ya Familia nchini Malawi!


Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 6 Novemba 2014 amewapongeza na kuwashukuru Maaskofu Katoliki kutoka Malawi wanaofanya hija ya kitume mjini Vatican, kwa sadaka na majitoleo yao kwa ajili ya kuwahudumia Watu wa Mungu nchini Malawi, kwa kujikita katika umoja; haki, amani na upatanisho; mambo msingi yanayoongoza mchakato wa Uinjilishaji wa kina, ustawi na maendeleo ya wananchi wa Malawi kwa ujumla.

Licha ya changamoto nyingi ambazo wananchi wa Malawi wanakabiliana nazo katika medani mbali mbali za maisha, lakini bado familia inapewa kipaumbele cha kwanza katika kuwafunda vijana katika maadili na utu wema; kwa kukazia upendo wa dhati, sadaka, uaminifu pamoja na kuendeleza mchakato wa Malawi katika ujenzi wa Jamii inayosimikwa katika mshikamano wa dhati.

Familia inakabiliwa na changamoto mbali mbali kwa nyakati hizi, Maaskofu kama Mababa na wachungaji wanaalikwa kulea, kulinda na kuimarisha familia mintarafu tunu msingi za kiimani, ili kuimarisha maisha na utume wa Kanisa ndani ya Familia. Baba Mtakatifu anawataka Maaskofu wa Malawi kuona ukweli kuhusu maisha ya ndoa na familia katika harakati za kutangaza Injili, ili familia nzima na makando kando yake ipate kuponywa na kuimarishwa na upendo unaobubujika kutoka katika Injili na kufundishwa na Mama Kanisa.

Baba Mtakatifu Francisko analitaka Kanisa nchini Malawi kujielekeza zaidi katika shughuli zake za kichungaji kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya familia, kwa kuponya na kuimarisha tunu msingi za maisha ya kifamilia; kwa kufundisha na kuinjilisha familia, hasa zile zinazokabiliana na matatizo, kinzani na changamoto mbali mbali, ili Kanisa liweze kustawi na Malawi kupata maendeleo zaidi.

Kwa kuwa na familia imara, Kanisa linaweza kupata Mapadre na Watawa ambao wako tayari kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa jirani zao pamoja na kuendelea kuimarisha ari na moyo wa shughuli za kimisionari, ili kuwajengea waamini wa Malawi uwezo wa kuinjilisha, ili hatimaye, kushirikisha utajiri huu kwa Kanisa zima, daima kwa kutafuta mema kwa ajili ya wengine, sanjari na kuimarisha upendo kwa Makanisa ambayo yana upungufu mkubwa wa wahudumu wa Injili.

Baba Mtakatifu anawataka Maaskofu kuwa karibu na Mapadre wao, kwa kuwasikiliza na kuwahudumia kwa upendo wa kibaba unaojikita katika sadaka binafsi. Mapadre watambue na kuonja upendo kutoka kwa Maaskofu wao, daima wakijitahidi kuwapatia majiundo makini yanayogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili; Waseminari na Watawa waandaliwe barabara ili kuweza kutekeleza majukumu na dhamana yao kwa ufanisi mkubwa, ili waweze kujisadaka kwa furaha, kama kielelezo cha ukomavu wa majiundo yao katika azma ya Uinjilishaji mpya kwa Malawi na Ulimwengu katika ujumla wake.

Baba Mtakatifu anawahimiza Maaskofu wa Malawi kuendelea kuwafunda vijana wa Malawi, kwa kuwapatia ukweli wa imani na furaha inayobubujika katika utekelezaji wa kanuni maadili. Vijana wahubiriwe kwa ari na moyo mkuu unaobubujika upendo kwa Kristo na Kanisa lake; kwa kuimarisha misingi ya familia bora ili kujenga haki na fadhila mbali mbali.

Baba Mtakatifu anawakumbuka kwa namna ya pekee wananchi wa Malawi wanaoogelea katika dimbwi la umaskini na wagonjwa wa Ukimwi, kwa kulitaka Kanisa kuendelea kuonesha mshikamano na upendo na wananchi hao, kwa njia ya mikakati ya kichungaji, sala na huduma makini, kwa kutambua kwamba, Kristo alikuja hapa duniani ili kuganga na kuwaponya watu, ili waweze kupata maisha mapya. Baba Mtakatifu anawapongeza Maaskofu kwa kuwa karibu na wagonjwa pamoja na maskini nchini Malawi.







All the contents on this site are copyrighted ©.