2014-11-05 14:33:51

Wapendeni na kuwaombea Wakleri, kielelezo hai cha uwepo endelevu wa Kristo kati ya watu wake!


Baba Mtakatifu Francisko Jumatano, tarehe 5 Novemba 2014 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican aliendelea na katekesi yake juu ya Kanisa ambalo Roho Mtakatifu analijalia karama mbali mbali, ili kusaidia mchakato wa ujenzi wa Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa.

Wakleri ni zawadi ya Roho Mtakatifu kwa Kanisa, kwani kwa njia ya Sakramenti ya Daraja Takatifu, Maaskofu, Mapadre na Mashemasi wanaalikwa kuongoza na kuchunga kundi la Kristo, kwa kutoa kipaumbele cha pekee kabisa katika maadhimisho ya Sakramenti zinazowajalia waamini maisha mapya katika Kristo.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Kanisa katika muundo wake ni la Kierakia na Mama; Wakleri wamewekwa wakfu ili kutoa huduma ya kimama katika maisha ya kiroho. Utume huu unajionesha kwa namna ya pekee kwa Maaskofu wanaotakiwa kuiongoza Jumuiya ya Kikristo kama kielelezo hai cha uwepo endelevu wa Kristo kati ya watu wake. Kama ilivyokuwa kwa Mitume ambao Maaskofu ni waandamizi wao, wanaunda urika na Baba Mtakatifu ambaye ni Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Baba Mtakatifu anasema, urika huu haujioneshi tu wakati wa maadhimisho ya Sinodi za Maaskofu kama ilivyokuwa wakati wa maadhimisho ya Sinodi maalum ya Maaskofu kwa ajili ya familia iliyohitimishwa hivi karibuni hapa mjini Vatican bali inajionesha pia katika umoja na mshikamano na Maaskofu kutoka sehemu mbali mbali za dunia katika maisha yao ya kila siku.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi kumwomba Yesu Kristo awajalie kuwa karibu naye pamoja na kati yao kwa njia ya utume wa Maaskofu, Mapadre na Mashemasi. Huu ni umoja wa Kanisa ambalo ni la Kierakia!

Baba Mtakatifu anawaombea waamini na mahujaji wote amani na kwamba, Roho Mtakatifu asaidie kuimarisha Jumuiya zao, kusali na kumtukuza Mungu kwa njia ya ushuhuda wa maisha na matendo mema kwa jirani. Anawataka waamini kusali kwa ajili ya kuwaombea Maaskofu wao ambao ni kielelezo cha imani na alama wazi ya uwepo wa Mungu kati yao, kwa kutambua kwamba, Uaskofu ni utume unaojipambanua kwa njia ya huduma na sadaka, kwa kufuata mfano wa Yesu Kristo mchungaji mwema na wala si ufahari na heshima.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini kuwaombea Wakleri wawe kweli ni mfano unaoonekana wa uwepo wa Kristo kati ya watu wake, chombo cha umoja na mshikamano; baraka na wokovu.

Baba Mtakatifu Francisko anaipongeza Familia ya Mungu nchini Poland kwa maandalizi ya maadhimisho ya "Siku ya Sita ya Mshikamano na Kanisa linaloteseka!, itakayoadhimishwa Jumapili ijayo, kwa kuungana kwa namna ya pekee na wananchi wa Syria. Anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuwa karibu na wote wanaodhulumiwa na kunyanyaswa sehemu mbali mbali za dunia. Waendelee kuwakumbuka kwa hali na mali.

Baba Mtakatifu Francisko akizungumza na Askofu mkuu Cesare Nosiglia wa Jimbo kuu la Torino pamoja na ujumbe wake, amesema kwamba, panapomajaliwa, hapo tarehe 21 Juni 2015 atafanya hija ya kiroho huko Torino, ili kwenda kutoa heshima yake kwa Sanda Takatifu pamoja na kuunganika na Familia ya Mungu huko Torino katika maadhimisho ya Jubilee ya Miaka 200 tangu alipozaliwa Mtakatifu Yohane Bosco.









All the contents on this site are copyrighted ©.