Ubinafsi ni sumu inayotishia ustawi na maendeleo ya familia
Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro
Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwenda kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Ufaransa wanaoendelea
na mkutano wao wa mwaka uliofunguliwa Jumanne tarehe 4 Novemba 2014 amewataka Maaskofu
kuendelea kuwatangazia Watu wa Mungu Injili ya Furaha; kwa kukuza na kudumisha moyo
na ari ya kimissionari.
Baba Mtakatifu anaitakia Familia ya Mungu nchini Ufaransa
maandalizi mema kwa ajili ya maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani utakaozinduliwa
Jumapili ya kwanza ya Kipindi cha Majilio, yaani tarehe 30 Novemba 2014. Ni mwaka
maalum wa faraja na matumaini kwa Familia ya Mungu.
Kwa namna ya pekee, Baba
Mtakatifu Francisko anawapongeza Maaskofu Katoliki kutoka Ufaransa kwa kuchagua mada
ambazo zinashuhudia utashi wa Maaskofu Katoliki Ufaransa wa kujenga Kanisa ambalo
malango yake yako wazi pamoja na kuwataka kuendelea kuonesha mshikamano wa upendo
na udugu na Wakristo wanaoishi huko Mashariki ya Kati.
Wakati huo huo, Askofu
Georges Pontier, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Ufaransa, katika hotuba yake
ya ufunguzi amekazia umuhimu wa familia kama chombo kinachohifadhi maisha, ambayo
kwa sasa yako hatarini kutokana na sheria zinazokumbatia utamaduni wa kifo, kwa kushinikiza
ndoa za watu wa jinsia moja pamoja na kuendekeza kifo laini. Ubinafsi, usawa wa kijinsia
na haki binafsi ni kati ya mambo yanayohataraisha tunu msingi za maisha ya ndoa na
familia nchini Ufaransa.
Baraza la Maaskofu katika mkutano wake utakaohitimishwa
hapo tarehe 9 Novemba 2014 wamgusia pia masuala ya kimataifa kama vile kinzani na
migogoro ya kivita inayoendelea huko Ucrain, Mashariki ya Kati, nyanyaso na dhuluma
za kidini sehemu mbali mbali za dunia.