Onesheni haki, huruma na ukarimu wa Mama Kanisa kwa wote wanaomkimbilia katika shida
na mahangaiko yao ya ndani!
Baba Mtakatifu Francisko kabla ya kutoa Katekesi yake, Jumatano asubuhi tarehe 5 Novemba
2014 amekutana na kuzungumza na wajumbe wanaoshiriki katika kozi maalum juu shughuli
zinazofanywa na Mahakama kuu ya Rufaa ya Vatican, kwa kuwataka wahusika kuhakikisha
kwamba, wanatenda haki kwa kuharakisha kutoa maamuzi ya kesi mbali mbali ambazo wanazofanyia
kazi.
Baba Mtakatifu anasema, ameunda Tume maaluma itakayoandaa kanuni msingi
katika masuala ya haki na upendo, ili kuwasaidia watu kupata maamuzi ya Kanisa kuhusiana
na masuala ya ndoa yanayofikishwa Mahakani hapo, kwa kuzingatia haki! Kesi za ndoa
zinazokatiwa rufaa zinachukua muda mrefu kiasi cha kuwakatisha watu tamaa pamoja na
ukweli kwamba, Mahakama hizi ziko mbali sana na maisha ya watu wa kawaida, hali inayogumisha
upatikanaji wa haki katika masuala ya ndoa. Mahakama kuu ya Rufaa inapaswa kutoa maamuzi
ya haki, ili kuwaweka watu huru na vifungo vya ndoa.
Baba Mtakatifu amewataka
wafanyakazi wa Mahakama kuu ya Rufaa kuwa makini zaidi ili wasimezwe na malimwengu
wakajikuta wanatumbukia katika rushwa, mambo yanayosababisha kashfa ndani ya Kanisa.
Wafanyakazi waoneshe ukarimu, haki na huruma ya Mama Kanisa kwa wale wanaomkimbilia
katika shida na mahangaiko yao ya ndani; wamepewa bure na wao wanapaswa kutoa bure,
kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya roho za waamini.