Askofu mkuu Josè Manuel Imbamba, msemaji mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Angola,
Sao Tome na Principè, katika mahojiano maalum na Radio ya Taifa nchini Angola anabainisha
kwamba, Kanisa Katoliki litaendelea kusimama kidete kulinda na kutetea tunu msingi
za maisha ya ndoa na familia kadiri ya mpango wa Mungu na kukataa kishawishi cha kutaka
kuiga mambo ya kigeni na hatimaye, kumezwa na malimwengu.
Askofu mkuu Imbamba
anasema, kuna mambo ambayo ni kinyume cha maadili na utu wema, lakini kwa baadhi ya
Jamii yameanza kuonekana kuwa ni mambo ya kawaida na wala hakuna tena soni kuona watu
wa jinsia moja wakiishi kwa pamoja kama bwana na bibi; mambo ambayo baadhi ya Jamii
wanataka kuyahalisha kwa kuyapigia debe, ili yakubalike! Hii si haki wala busara!
Upendo kati ya Bwana na Bibi hauna budi kulindwa na kudumishwa kwani hapa
ni mahali patakatifu ambapo uhai wa mwanadamu unapata chimbuko lake, tayari kushiriki
katika kazi ya uumbaji, ambayo Mwenyezi Mungu amemdhamisha mwanadamu. Familia kadiri
ya mpango wa Mungu haina budi kukuzwa na kudumishwa, kwa kuwasaidia na kuwasindikiza
wanandoa watarajiwa na wanandoa wapya katika hija ya maisha yao, wanapojitahidi kujenga
familia kama Kanisa dogo la nyumbani.
Wanandoa wapate msaada kutoka ndani
ya Kanisa, ili kuimarisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia zinazojikita katika
upendo usiogawanyika, udumifu, uaminifu, majadiliano, heshima; huruma na msamaha pamoja
na ukuaji wa mtu mzima: kiroho na kimwili.