2014-11-05 07:13:05

Cheche za Sinodi zilivyoutikisa ulimwengu!


Kwa mara ya kwanza katika historia ya maadhimisho ya Sinodi za Maaskofu, Sinodi maalum kwa ajili ya Familia imekuwa na mvuto, changamoto na tafakari za kina, kwani maisha ya ndoa na familia ni mambo yanayowagusa wote, kila mtu kwa kadiri ya nafasi na dhamana yake ndani ya Jamii. Baba Mtakatifu Francisko ameshiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Sinodi maalum ya Maaskofu kwa ajili ya familia iliyofunguliwa hapo tarehe 5 hadi tarehe 19 Oktoba 2014. RealAudioMP3

Baba Mtakatifu aliguswa na mchango wa Mababa wa Sinodi iliyokuwa inatolewa kwa kuzingatia: ukweli, uwazi, uzoefu na mang’amuzi ya shughuli za kichungaji kwa ajili ya familia sehemu mbali mbali za dunia. Baba Mtakatifu wakati wote ameonesha hali ya utulivu, huku akisikiliza kwa makini na kuhimiza ukweli na uwazi, mambo msingi yatakayoliwezesha Kanisa kuibua mbinu mkakati wa shughuli za kichungaji kwa ajili ya familia, wakati wa maadhimisho ya Sinodi ya kawaida ya Maaskofu itakayofanyika mjini Vatican kuanzia tarehe 4 hadi tarehe 25 Oktoba 2015.

Padre Federico Lombardi, Msemaji mkuu wa Vatican anabainisha kwamba, maadhimisho ya Sinodi maalum ya Maaskofu kwa ajili ya Familia ni hija ndefu ambayo itafanyika kwa kipindi cha miaka miwili, kwani ni “Sinodi nyeti” inayogusa masuala tete yanayojikita katika Sheria za Kanisa na Mafundisho tanzu ya Kanisa. NI Sinodi inayogusa maisha na utume wa Kanisa kwa kuwashirikisha kwa namna ya pekee kabisa waamini walei, pamoja na viongozi wa Kanisa; ili kwa pamoja waweze kupata dira na mwelekeo wa maisha ya kichungaji kwa ajili ya familia. Hapa Kanisa linataka kutembea kwa kuendelea kutangaza Injili ya Familia, kama walivyofanya Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican. Kuna matatizo, changamoto na fursa ambazo Mama Kanisa, anapaswa kuzifanyia kazi kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya familia.

Padre Lombardi anasema, maandalizi ya maadhimisho ya Sinodi maalum ya Maaskofu kwa ajili ya familia yalianza kwa kutuma maswali dodoso kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema; Baba Mtakatifu akaitisha mkutano maalum wa Makardinali ili kujadili kuhusu utume wa Kanisa kwa ajili ya familia na hatimaye, Mabaraza ya Maaskofu Kikanda na Kitaifa yakapata fursa ya kujadili na mwishoe, Hati ya Kutendea kazi kwa ajili ya Mababa wa Sinodi ikatolewa.

Sinodi ambayo maana yake ni kutembea kwa pamoja, imewashirikisha watu wengi ili kupata mwelekeo wa shughuli za kichungaji kwa kujikita katika Mafundisho Tanzu ya Kanisa. Kila jambo lilifanyika kadiri ya mpango wa Kanisa na wala hakuna kitu ambacho kilitolewa kwa kushtukiza.

Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri na hotuba yake ya ufunguzi wakati wa maadhimisho ya Sinodi, aliwataka Mababa wa Sinodi kuzunguza kwa kuzingatia ukweli na uwazi; uhuru pasi na wasi wasi, kama misingi madhubuti ya mchakato wa majadiliano ya Sinodi. Wakati wote alikaa kimya na kuwasikiliza Mababa wa Sinodi wakijadili na mwishoni, akawashirikisha uzoefu na mang’amuzi yake wakati wa maadhimisho ya Sinodi maalum ya Maaskofu kwa ajili ya familia, kwa kuiwezesha Sinodi kubaki katika mwelekeo wake wa kiimani, tayari kuwatangazia Watu wa Mataifa Injili ya Familia.

Baba Mtakatifu alikuwa ni mhimili mkuu wa umoja na mshikamano wakati wote wa maadhimisho ya Sinodi, ameonesha utulivu wa ndani hata pale ambapo watu walidhani kwamba, Kanisa linameguka. Ajiweka chini ya usimamizi na maongozi ya Roho Mtakatifu, kwa ajili ya mafao na ustawi wa Kanisa la Kristo. Ameliwezesha Kanisa kufanya mang’amuzi ya kina, ili Kanisa liweze kupata mwelekeo sahihi kwa ajili ya Injili ya Familia.

Padre Lombardi anasema, Hati Elekezi kutoka kwa Mababa wa Sinodi ilipata mwangwi mkubwa kutoka kwenye vyombo mbali mbali vya habari, lakini kwa masikitiko makubwa, baadhi ya vyombo hivi vilipotosha ukweli kwa ajili ya mafao yao binafsi. Majadiliano ya Mababa wa Sinodi katika makundi madogo madogo yameweza kuboresha hati elekezi na hatimaye kupata Hati ya Sinodi ambayo Baba Mtakatifu Francisko amekabidhiwa tayari kutumwa kwa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki kama hati ya majadiliano.

Vyombo vingi vya mawasiliano ya jamii vilijikita katika mada ya wanandoa walioachana na baadaye kuamua kuoa au kuolewa tena na uwezekano wa kushiriki katika Sakramenti za Kanisa pamoja na swala tete la ndoa za watu wa jinsia moja, lililopigiwa debe kiasi hata cha “kutibua nyongo” miongoni mwa Familia ya Mungu. Lakini watu wameweza kufahamishwa kwa kina na mapana yale yaliyojadiliwa na Mababa wa Sinodi.

Padre Lombardi anasema, Sinodi hii imeliwezesha Kanisa kutembea kwa pamoja ili kutafuta mapenzi ya Mungu minaytafu mwanga wa Injili na Imani ili kuibua mikakati itakayoliwezesha Kanisa kuihudumia Familia kwa kusoma alama za nyakati. NI matumaini ya Padre Lombardi kwamba, Familia ya Mungu itaweza sasa kushiriki kikamilifu tena ili kuweza kupata mwelekeo mpya katika maadhimisho ya Awamu ya Pili ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Familia.

Imehaririwa na
Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.