Suala ya wahamiaji na wakimbizi Barani Ulaya ni tete na nyeti!
Padre Tumaini Litereku, kutoka Jimbo kuu la Songea, Tanzania ambaye kwa sasa anasoma
nchini Ujerumani katika mahojiano maalum na Radio Vatican anabainisha kwamba, suala
la wakimbizi na wahamiaji kutoka Barani Afrika wanaotafuta hifadhi na ubora wa maisha
ni tete na nyeti, linahitaji kuangaliwa kwa mapana zaidi, kwani mambo yanazidi kubadilika
kila kukicha!
Kuna baadhi
ya watu wanadhani kwamba wakishapata fursa ya kutia mguu Barani Ulaya, mambo yao yatakuwa
yamewanyookea na hapo umaskini wataupatia kisogo na kuanza kupeta kwa kula kuku kwa
mrija! Lakini, ukweli na uzoefu wa mambo unaonesha kwamba, licha ya mafanikio makubwa
yanayoonekana Barani Ulaya na kwingineko ni matokeo ya mchakato mkubwa katika maisha
ya watu. Watu wasidhani kwamba, kwa kuzamia meli au kwa kutafuta njia za mkato ili
kufika Ulaya ni tiketi ya mafanikio. Kuna watu wanateseka na utu wao kudhalilishwa
kutokana na ndoto kama hizi.
Padre Litereku anasema, pale inapowezekana watu
wajitahidi kutafuta na kuboresha maisha yao kwa juhudi na maarifa wakiwa ndani ya
nchi zao wenyewe, kwani hii ni haki yao msingi. Ni wajibu wa Serikali husika kuhakikisha
kwamba, zinaweka mazingira mazuri kwa wananchi wao ili waweze kufaidika kwa fursa
mbali mbali zinazopatikana ili kujiletea maendeleo endelevu. Ili kufikia lengo hili,
wahenga waliwahi kusema kunahitajika: siasa safi, uongozi bora na ardhi.
Zama
za kuzamia meli kwa ajili ya kutafuta maisha bora Barani Ulaya kwa sasa zimepitwa
na wakati, kwani huu ni mwanzo wa kuweka maisha rehani, kwani si mchezo watu wanazama
na kufa maji baharini; watu wanadhulumiwa na kunyanyaswa na pale wachache wanapofaulu
kufika Ulaya wanajikuta wamefungiwa kwenye kambi za wakimbizi na wahamiaji na hapo
ndiyo mwisho wa ndoto ya kula kuku kwa mrija wakiwa Ulaya, kwani hali inakuwa ni mbaya
zaidi kuliko hata pengine walivyoiacha katika nchi zao za asili.
Padre Tumaini
Litereku, watu wajitahidi kubaki na kutafuta riziki na maisha bora zaidi katika nchi
zao wenyewe. Kwa wale wanaotaka kutafuta riziki ya kijani kibichi Ulaya, basi watumie
njia halali na kwa kuzingatia sheria, vinginevyo watajikuta wakidhalilishwa na hatimaye
kupoteza matumaini ya maisha!