Mshikamano wa Baba Mtakatifu kwa wananchi wanaoteseka huko Mashariki ya Kati!
Askofu mkuu Giovanni Pietro Dal Toso, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa linaloratibu
misaada ya Kanisa Katoliki, Cor Unum baada ya ziara yake ya kikazi nchini Syria anasema,
hali bado ni tete kwa wananchi wengi wa Syria baada ya vita kuendelea kurindima nchini
humo kwa miaka mitatu sasa. Kanisa litaendelea kuonesha mshikamano wa upendo kwa wote
wanaoteseka kutokana na vita pamoja na kinzani za kijamii kwa kushirikiana na Kanisa
mahalia katika kuwahudumia watu kwa hali na mali.
Akiwa nchini Syria, Askofu
mkuu Dal Toso, amepata nafasi ya kukutana na kuzungumza na viongozi mbali mbali wanaoratibu
misaada kwa ajili ya wananchi wa Syria. Ameshiriki pia katika mkutano wa Baraza la
Maaskofu Katoliki Syria ambao wameiomba Jumuiya ya Kimataifa kusitisha kabisa biashara
ya silaha kwa Syria kwani ni chanzo cha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Maaskofu
wamewataka pia Wakristo kushinda kishawishi cha kutaka kukimbia kutoka huko Mashariki
ya Kati.
Askofu mkuu Dal Toso anasema, hadi sasa kuna jumla ya wakimbizi na
wahamiaji millioni kumi kutoka Syria wanaohitaji msaada wa dharura, kwani ni watu
ambao wameathirika kwa kiasi kikubwa na madhara ya vita na kinzani za kijamii. Kuna
umati mkubwa wa watu ambao hauna fursa za ajira; watu wanaendelea kutumbukizwa katika
umaskini wa hali na kipato pamoja na magonjwa; shule zinashindwa kutoa elimu kwa kuhofia
usalama wa maisha ya wanafunzi, jambo ambalo ni hatari kwa kizazi kijacho.
Askofu
mkuu Dal Toso anasema, ziara yake ya kikazi nchini Syria ililenga pamoja na mambo
mengine kuonesha mshikamano na Kanisa mahalia pamoja na kuwatia shime Mashirika ya
misaada, ili yaendelee kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji kwa ari na moyo mkuu pasi
ya kukata tamaa. Cor Unum imeliwezesha Kanisa nchini Syria kuwahudumia watu zaidi
ya millioni moja na nusu wanaoishi huko Syria, Lebanon, Yordani na Uturuki.
Wananchi
kwa namna ya pekee, wanamshukuru Baba Mtakatifu Francisko na Kanisa kwa ujumla kwa
kuonesha mshikamano wa upendo katika shida na mahangaiko yao ya kila siku. Wanapenda
kutoa mwaliko kwa pande zote zinazohusika kuanza tena mchakato wa majadiliano na upatanisho
wa kitaifa, ili amani na utulivu viweze kurejea tena nchini Syria.