2014-11-04 12:02:46

Jitokezeni kupiga kura hapo tarehe 7 Desemba 2014, kamwe msifanye mzaha!


Baraza la Maaskofu Katoliki Mauritius linawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kushiriki kikamilifu katika zoezi la kupiga kura litakalofanyika tarehe 7 Desemba 2014, kwa kuwajibika barabara pamoja na kutoa kipaumbele cha kwanza kwa mafao ya wengi, haki, amani na utulivu. Wanasiasa kwa upande wao, hawana budi kuendesha kampeni kwa ustaarabu na utulivu ili kuweza kunadi vyema sera zao, zitakazowashawishi wananchi kuwapatia ridhaa ya kuongoza nchi.

Baraza la Maaskofu linawasihi waamini na wananchi kwa ujumla kushiriki kikamilifu katika zoezi zima la kupiga kura na kuacha tabia ya kususia uchaguzi kwani hii ni haki yao msingi na wanapaswa kutekeleza wajibu wao kama raia kwa kupiga kura ili kuwachagua viongozi wanaowataka.

Wananchi watambue kwamba, kwa njia ya kura makini, wanaweza kuchagua hatima na mwelekeo wa nchi yao kwa siku za usoni; kwa kuzingatia sera makini katika sekta ya elimu, afya, utunzaji bora wa mazingira; mapambano dhidi ya baa la umaskini; mshikamano na umoja wa kitaifa pamoja na matumizi bora na sahihi ya fedha na rasilimali ya nchi, kwa ajili ya mafao ya wengi.

Wananchi washiriki kikamilifu ili kweli siasa iweze kuwa na mwelekeo chanya, ikilinganishwa na hali ya sasa ambapo wanasiasa wengi hawana tena mvuto na mashiko miongoni mwa wananchi, kwani wanaonekana kuchoka na kufilisika kimaadili na kiutu. Wananchi wapige kura ili kuwakataa wanasiasa uchwara na walevi wa madaraka; wanasiasa wezi na mafisadi. Vyama vya siasa vioneshe sera makini kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wananchi wote; kwa kuwa na uwezo wa kufanya maamuzi magumu kwa ajili ya mustakabali wa nchi.

Wananchi wamechoka kusikia kila mwaka ahadi hewa zisizotekelezeka hata kidogo, bali wananchi waoneshwe mikakati endelevu katika maboresho ya maisha ya watu: kijamii, kisiasa, kiuchumi na katika kupambana na uharibifu mkubwa wa mazingira!







All the contents on this site are copyrighted ©.