2014-11-04 07:35:34

Familia za Kikristo ni kitalu cha miito mitakatifu ndani ya Kanisa!


Askofu mkuu Protase Rugambwa, Katibu Mwambata wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu ambaye pia ni Rais wa Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa katika mahojiano maalum na Radio Vatican anabainisha kwamba, kimsingi, Familia za Kikristo zinapaswa kuwa ni chemchemi ya miito mitakatifu ndani ya Kanisa, kitalu cha kukuza na kuendeleza ari na moyo wa kimissionari, ili kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kutangaza Injili ya Furaha hadi miisho ya dunia. RealAudioMP3

Askofu mkuu Rugambwa anasema, Familia zinawajibika kukuza na kulea miito mbali mbali ndani ya Kanisa, lakini kwa namna ya pekee, miito ya Kipadre na Kitawa, kwani hii ni mihimili mikuu ya Uinjilishaji. Kuna baadhi ya Makanisa mahalia miito inaendelea kuchanua kama "Mtende wa Lebanon", lakini kuna baadhi ya Makanisa, miito inaendelea kunyauka kama "ardhi kavu isiyokuwa na maji". Lakini, Makanisa mahalia yanachangamotishwa kushirikiana kwa karibu zaidi katika kuendeleza kazi za kimissionari sehemu mbali mbali za dunia.

Askofu mkuu Rugambwa anasema, vijana wanapaswa kufundwa na kuhimizwa kujisadaka kwa ajili ya kushiriki katika mchakato wa uenezaji wa Ufalme wa Mungu unaojikita katika misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano kati ya watu. Moyo wa kimissionari hauna budi kupata chimbuko lake kutoka katika familia, kwa kutambua kwamba, familia ni Kanisa dogo la nyumbani, ni kitalu cha kukuza na kulea miito.

Hata katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia, vijana waendelee kuhamasishwa kujiunga na wito wa Kipadre na Kitawa ili kushiriki kikamilifu katika mchakato wa Uinjilishaji mpya, dhamana inayofanyiwa kazi na Mama Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo. Waamini washiriki kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao kumtangaza Mwenyezi Mungu kwa njia ya Yesu Kristo, ili kuonesha imani tendaji.







All the contents on this site are copyrighted ©.