2014-11-03 08:29:53

Viongozi wachovu na walevi wa madaraka wamekumbana na nguvu ya umma nchini Burkina Faso!


Baraza la Maaskofu Katoliki Burkina Faso linasema, machafuko ya kisiasa nchini humo ni matokeo ya kukithiri kwa rushwa na ufisadi uliokuwa unafanywa na baadhi ya wanasiasa wasiokuwa na uzalendo wala machungu ya mahangaiko ya watu wao. Haya pia ni maendeleo ya sayansi na teknolojia ya habari ambayo inatumiwa na vijana wengi katika mchakato wa kuhabarishana, katika misingi ya ukweli na uwazi. Vijana wengi wamechoshwa na hali inayoendelea nchini mwao na hivyo kwa sasa viongozi wa kisiasa wanaiona nguvu ya umma.

Maaskofu Katoliki Burkina Faso wanasema, tangu mwaka 1985 idadi ya watu wasiojua kusoma wala kuandika imeongezeka maradufu kutoka asilimia 16. 17% hadi kufikia asilimia 32%. Katika miaka ya hivi karibuni kumekuwepo na maendeleo makubwa ya vyombo vya mawasiliano ya kijamii, kiasi kwamba, watu wanapata habari nyingi, ikilinganishwa na miaka kadhaa iliyopita. Maaskofu wanasema hapa kuna maendeleo ya vitu lakini watu wanaendelea kuogelea katika dimbwi la umaskini wa hali na kipato na kwamba, pengo kati ya maskini na matajiri linazidi kuongezeka maradufu.

Utajiri wa nchi unamilikiwa na kundi la watu wachache hali ambayo imesababisha manung'uniko miongoni mwa raia wa Burkina Faso. Kundi hili wanasema Maaskofu limekuwa na nguvu kubwa ya kifedha kiasi kwamba, wakati huu rushwa inatembezwa wazi wazi na kwamba, ubadhirifu wa mali ya umma umefikia kiwango cha hali ya juu kabisa.

Baadhi ya viongozi wa kisiasa wameanza kulewa madaraka kiasi hata cha kutaka kupindua Katiba ya nchi kutokana na uchu wa madaraka, matokeo yake wanasiasa wachovu wamekiona cha mtema kuni kwa kukumbana na nguvu ya umma. Baraza la Maaskofu Katoliki Burkina Faso linawataka wananchi kutulizana na kudumisha amani na usalama wakati huu wa kipindi cha mabadiliko!







All the contents on this site are copyrighted ©.