Utunzaji bora wa mazingira ni suala linalogusa haki na kanuni maadili
Mapambano dhidi ya baa la umaskini pamoja na utunzaji bora wa mazingira ni kati ya
mambo msingi yanayopaswa kufanyiwa kazi na Jumuiya ya Kimataifa mara baada ya kuhitimisha
utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo ya Millenia ifikapo mwaka 2015. Dunia inakabiliwa
na madhara makubwa yanayosababishwa na mabadiliko ya tabianchi, mambo yanayochangiwa
kwa kiasi kikubwa na ulaji wa kupindukia pamoja na uzalishaji mkubwa wa hewa ya ukaa
kutoka katika viwanda.
Askofu mkuu Bernadito Auza, Mwakilishi wa kudumu wa
Vatican kwenye Umoja wa Mataifa anasema kwamba, ujumbe wa Vatican unaliangalia suala
hili si tu katika miwani ya mazingira bali ni suala linalogusa haki na kanuni maadili,
kwa kuwasaidia maskini wanaoathirika zaidi kutokana na madhara ya mabadiliko ya tabianchi
sanjari na kuwajengea uwezo wa kuwa na teknolojia rafiki, itakatoweza kudhibiti uchafuzi
wa mazingira.
Jumuiya ya Kimataifa inaanza kuelekeza macho yake kwenye mikutano
mikubwa ya kimataifa itakayofanyika hapo mwakani 2015, ambako Jumuiya ya Kimataifa
inatarajiwa kupata muafaka wa makubaliano juu ya udhibiti wa uzalishaji wa hewa ya
ukaa, kwa kutambua kwamba, kila mtu anawajibika kwa kiasi chake, kulinda na kutunza
mazingira. Hii inatokana na ukweli kwamba, ulimwengu kwa sasa unaonekana kama kijiji
na hivyo unahitaji uwajibikaji wa pamoja, kwa ajili ya usalama na ustawi wa watu kwa
sasa na kwa siku zijazo.
Changamoto ya utunzaji bora wa mazingira inahitaji
siasa safi na mikakati makini ya kiuchumi, itakayotekelezwa na Jumuiya ya Kimataifa,
kwa kuzingatia ukweli wa tafiti za kisayansi; kwa kuelewa na kutekeleza mikakati itakayopangwa
kama sehemu ya agano la kimaadili ili kutunza mazingira. Kila mtu anapaswa kutekeleza
wajibu wake kadiri ya uwezo na fursa alizo nazo, ili dunia iweze kuwa ni mahali pazuri
zaidi pa kuishi.