2014-11-03 07:31:46

Ugonjwa wa Ebola unaendelea kusababisha maafa makubwa kwa watu!


Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis, tarehe 4 Novemba 2014 linafanya mkutano wa kimataifa, ili kubainisha mbinu mkakati utakaotumiwa na Mashirika ya misaada ya Kanisa Katoliki kwa ajili ya kuwasaidia watu walioathirika kutokana na ugonjwa wa Ebola, Afrika Magharibi.

Mkutano huu unawashirikisha mabingwa na wataalam wanofanya kazi na Kanisa Katoliki katika sekta ya afya, ili kuweza kukabiliana kikamilifu na janga la ugonjwa wa Ebola ambalo kwa sasa ni janga la kimataifa. Mashirika ya misaada yameendelea kuwa bega kwa bega na waathirika wa ugonjwa wa Ebola kwa kuwapatia msaada wa hali na mali.

Juhudi kwa sasa anasema Monsinyo Robert J. Vitillo, Afisa wa Caritas Internationalis anayeshughulikia masuala ya afya, juhudi zinaelekezwa si tu katika kudhibiti kuenea kwa ugonjwa wa Ebola bali kuwasaidia hata wale ambao wameathirika kutokana na ugonjwa wa Ebola, kwa kuwekeza zaidi katika sekta ya afya ili kupambana na magonjwa mengine pia.

Ugonjwa wa Ebola ambao kwa sasa ni tishio kwa nchi za Afrika Magharibi umetikisa: sekta ya elimu, afya, uchumi, siasa na maisha ya kiroho, hasa zaidi mijini. Licha ya ugonjwa wa Ebola kwa sasa kuwa ni janga la kimataifa, lakini bado watu wengi wanaendelea kupoteza maisha kutokana na ugonjwa wa Malaria, Ukimwi pamoja na wanawake wajawazito wakati wa kujifungua. Watu wanafariki dunia kutokana na njaa kwani usambazaji wa chakula umeathirika kwa kiasi kikubwa.








All the contents on this site are copyrighted ©.