2014-11-03 13:55:30

Ufufuko ni kiini cha imani ya Kanisa inayofumbata ukweli na maisha ya uzima wa milele


Liturujia ya Neno la Mungu katika Ibada ya kuwakumbuka na kuwaombea Makardinali na Maaskofu waliofariki dunia katika kipindi cha mwaka 2013- 2014 ilijikita katika imani katika Fumbo la Ufufuko, ukweli unaojionesha tangu katika Agano la Kale na kupata utimilifu wake katika Agano Jipya.

Ni majadiliano ya kina kati ya Mwenyezi Mungu na Watu wake katika hija ya maisha yao katika historia. Fumbo la Ufufuko limefahamika kwa kina zaidi katika Agano Jipya, Yesu mwenyewe alipowaambia wafuasi wake kwamba, Yeye ni ufufuko na Uzima, kwani hapa Fumbo la Ufufuko linamwilishwa kikamilifu na kuwa ni ukweli mfunuliwa.

Haya yamesemwa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Ibada ya Misa Takatifu iliyofanyika kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, kwa ajili ya kuwaombea Makardinali na Maaskofu waliofariki dunia hivi karibuni. Baba Mtakatifu anasema, Neno la Mungu linaonesha simulizi kuhusu kifo cha Yesu na Kaburi tupu, hitimisho la hija ya Watu wa Mungu linalozima kiu ya udadisi wa binadamu.

Baba Mtakatifu anasema, huu ni mwaliko wa kuingia na kushiriki katika tukio hili, kwa kusimama kwanza kabisa mbele ya Msalaba, kama alivyofanya Bikira Maria, wale wanawake pamoja na yule Askari, ili kusikiliza kilio cha Yesu, wakati akitoa pumzi yake ya mwisho na baadaye kufuatia kimya kikuu, kinachojidhihirisha Jumamosi kuu.

Baada ya hapo waamini wanaalikwa mapema asubuhi kwenda kushuhudia mbiu ikitangaza kufufuka kwa Yesu, jibu makini, kiini na msingi wa imani kwa Yesu aliyeteswa Msalabani, akafa na kufufuka. Hiki ndicho kiini cha mahubiri ya Mtakatifu Paulo na kiini cha imani ya Kanisa inayofumbata ukweli na maisha ya uzima wa milele.

Hivi ndivyo Baba Mtakatifu Francisko alivyowakumbuka Makardinali na Maaskofu waliofariki dunia katika kipindi cha miezi kumi na miwili iliyopita; ni viongozi ambao wameacha kumbu kumbu ya kudumu na ushuhuda katika kulihudumia Kanisa. Ni watu waliofahamika na wengi, lakini wengi wao wanauangalia uso wa Mungu, mwingi wa huruma na mapendo; wanaungana na Bikira Maria anayewaombea watoto wake wapendwa, ili wakiwa wameungana na waamini waliowahudumia hapa duniani waweze kupata furaha inayobubujika kutoka kwa Yerusalemu mpya.







All the contents on this site are copyrighted ©.