2014-11-03 10:40:06

"Mkiona yamechacha, itisheni Mtaguso wa Familia"!


Mpendwa Msikilizaji wa Kipindi chetu cha Kanisa la nyumbani, Tumsifu Yesu Kristo! Karibu katika kipindi chetu pendevu tuendelee kupyaishana juu ya yale yaliyojiri katika Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. RealAudioMP3

Lengo letu: Mtaguso utue vizuri katika familia na maisha yako, ili tuuishi katika maisha yetu ya kila siku. Miongozo ya Mtaguso ndiyo dira ya kufuata ili sote kama waana wa Kanisa twende pamoja. Jumuiya yoyote ile ya watu isiyokuwa na miongozo thabiti, hukosa mwelekeo na mwisho huwa ni kambi ya fujo. Ili kulipatia Kanisa mwelekeo sahihi kwa nyakati mbalimbali, Mamlaka halali ya Kanisa na kwa utaratibu maalumu, hutupatia miongozo ya kuifuata ili tuweze kufikia lengo. Haswaa, ndiyo ilivyokuwa kwa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican. Ndiyo maana mpendwa msikilizaji, tunakumbushana kile tulichoagizwa, ili nyakati zetu hizi zenye kelele nyingi, tusipoteze mwelekeo. Twende pamoja, tukafike salama bandarini pa Yesu.
Leo “tuidonoe” kwa umbali, hati ya Mwanga wa Mataifa ambayo ni Katiba. Hati hiyo juu ya Kanisa ndiyo muhimu kuliko nyingine zote za mtaguso, ndiyo maana tunakuta imesheheni mambo mengi hata yale yaliyomo katika hati nyinginezo pia. Inajibu swali la Mwenyeheri Papa PauloVI, lililouliza, “Kanisa, unasemaje juu yako?”. Katika hati hii, Kanisa linajieleza, linajifafanua, linajidhihirisha undani wake na utume wake na nafasi yake zaidi katika Ukombozi wa Mwanadamu.

Sura ya kwanza inafafanua fumbo la Kanisa kama sakramenti. Kwa nje linaonekana katika muundo wa jamii ya watu na kwa ndani limebeba neema zisizoonekana kwa macho. Ndani ya Kanisa Mungu anaishi na kufanya kazi. Na ndiyo maana twasema kwa njia ya Kanisa tunapata neema, kwa sababu Kanisa ni chombo cha neema za Mungu. Tunaelezwa pia jinsi Baba, Mwana na Roho Mtakatifu wanavyohusika na Kanisa. Hati hii inalieleza Kanisa kama kundi la kondoo, shamba, jengo na hekalu la Mungu au bibiarusi anayeungana na Bwanaarusi wake kuwa mwili mmoja, yaani mwili wa Kristo. Wazee wetu wa Mtaguso walitumia lugha za picha ili kutusaidia sisi kuelewa zaidi fumbo la Kanisa.

Sura ya pili inaeleza jinsi watu wanavyohusika na fumbo la Kanisa. Kwa njia ya sakramenti sote tumefanywa kuwa taifa mmoja la Mungu. jinsi ambavyo katika Agano la Kale Mungu mwenyewe aliliridhia kuwaokoa watu kama taifa na siyo mtu mmoja mmoja, hali kadhalika sasa Mungu anatuokoa sote kwa njia ya Kanisa kama taifa lake takatifu. Katika taifa hilo watu wote wanapaswa kuingia bila ya ubaguzi ili wawe kitu kimoja. Ndiyo maana linaitwa katoliki, yaani la watu wote, wa mahali pote na nyakati zote.

Pamoja na mafundisho hayo, yapo pia mafundisho mengine yanayoleta uzito katika sura nzima ya Kanisa katika muundo wale na katika Imani yake. Kuna mafundisho kuhusu muundo wa uongozi wa Kanisa, hasa uaskofu. Tunafundishwa kwamba kama vile mitume walivyokuwa kundi moja na Petro akiwa kiongozi wao, maaskofu wote pia ni kundi moja (kwa sababu ndiyo warithi wa mitume) na Askofu wa Roma yaani Baba Mtakatifu, mrithi wa Mtume Petro na wakili wake Yesu Mwenyewe, ndiyo Kiongozi na Mkuu wa Maaskofu hao na Kanisa zima. Mtaguso huu, umesisitiza pia umoja wa maaskofu, ukielekeza kila mmoja wao afanye kazi yake akishirikiana na kundi lote la waamini na achangie ustawi wa Kanisa zima, si jimbo lake tu. Kinachosisitizwa hapa ni umoja na ushirikiano katika uongozi wa Kanisa, na pia kumtazama jirani pia. Ubinafsi ni aina ya uchoyo mharibifu.

Sehemu hii ndiyo inafungua dirisha kwa Kanisa letu la nyumbani yaani familia. Kama tulivyosikia na tutaendelea kusikia tena na tena, Familia ni Kanisa la Nyumbani. Ili kanisa hilo dogo la nyumbani liweze kustawi vema, linahitaji miongozo na uongozi thabiti. Miamba mikuu miwili ya usitawi wa Kanisa la nyumbani ni Baba na Mama. Na ili Baba na Mama ambao wameungana kwa wito maalumu wa ndoa waweze kutimiza wajibu wao vizuri, wanahitaji kuwa na Umoja wenye upamoja na ushirikiano kati yao. Baba na Mama wajitahiti kuwa na kauli mmoja kwa maslahi na usitawi wa familia. Inapotokea kwamba baba na mama wamegawanyika, hawasikilizani katika masuala ya msingi ya familia, hapo wajue wazi kuwa wanaligawanya Kanisa la nyumbani.

Jinsi ambavyo Mtaguso unasisitiza umoja kati ya Askofu na Kanisa analolisimamia, na sisi leo tunataka kusisitiza sana umoja kati ya wazazi na watoto, umoja ndani ya familia. Usitawi wa familia huwa hauletwi tu na fanaka za mali na vipaji walivyonavyo wanafamilia. Roho ile ya umoja, ndiyo inayojenga familia. Na umoja wa kweli uliyositawi ndani ya familia, huwa na matunda mema kwa jirani. Familia yetu inaponeemeka na kusitawi sana, tusisahau kuwa sisi ni sehemu ya mwili wa fumbo wa Kristo kama walivyo na familia nyinginezo pia. Hivi kama familia tuna wito pia wa kuchangia amani na usitawi wa familia nyinginezo, kwa sala, ushauri mwema na matendo ya upendo. Haileti furaha kwetu kama sisi wanafamili tunafikiri kuwa tunaishi kwa amani na starehe zinazokaribiana na anasa, na wakati familia zote zinazotuzunguka wanapiga miayo mirefu ya njaa na magonjwa na kila adha. Umoja na usitawi wetu, utukumbushe kumtazama jirani. Jirani akisitawi, sisi kama familia tutafurahi zaidi na tutakuwa na amani zaidi.

Nyakati zetu hizi, pamoja na mambo mengine mengi, mchwa mbaya sana unaotafuna familia nyingi ni mtengano na ukorofi-katiri uliyopo katika ya baba na mama. Wazazi kama viongozi wa familia, wakikikosa umoja tu, hata watoto pia watakosa umoja. Kwa lazima, watatokea watoto wa baba, na watoto wa mama. Baba atalazimisha watoto wamchukie mama yao na mama atalazimisha watoto wamchukie baba yao.

Mwishoni mwa siku, familia nzima inakuwa sio kanisa la nyumbani tena bali ni sumu kwa majirani na sumu kwa Kanisa zima. Inakuwa ni kambi ya kuunda watu wenye hasira, wakali na waliojikatia tamaa. Katika hali hiyo, hata shughuli za uzalishaji mali pia zitakosa unadhifu kwa sababu kutakuwa na miradi ya baba na miradi ya mama. Hakuna miradi ya familia, kisa? Wazazi wamekosa umoja. Hatimaye mali hizo inakuwa ni mwendelezo wa fujo zaidi ndani ya familia.

Kumbe mpendwa msikilizaji, tunapotafakari juu ya hadhi ya Kanisa na Muundo wa Kanisa mintarafu uongozi, tusisahau kujiuliza na kujielekeza maswali haya: Tunataka familia yetu iwe ya namna gani. Swali hili linajibiwa na wanafamilia wote. Na baada ya hapo, sisi kama familia, utume wetu kwa familia majirani ni upi? Tunafanya nini katika kuchangia usitawi wa familia za wenzetu? Endapo tutajikuta kama familia tumepindapinda kidogo, basi tujipe ujasiri, tuitishe mtaguso wa kifamilia, ili tujitambue, tujikosoe, tujipe maana chanya zaidi na mwelekeo mzuri. Kwa njia hiyo tutakuwa kweli tunashikiri fumbo na utume wa Kanisa na papo hapo kama Kanisa lilivyo Mwanga kwa Mataifa, familia yetu nayo itakuwa Nuru kwa majirani wote. Na iwe hivyo!!
Kutoka katika Studio za Radio Vatican, ni mimi Padre Pambo Martin Mkorwe OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.