Kifo si kigingi cha maisha ya binadamu, kwani binadamu ameumbwa na Mwenyezi Mungu
ili aweze kufurahia maisha yenye uzima wa milele. Ni maneno ya Baba Mtakatifu Francisko
wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro
mjini Vatican, Jumapili tarehe 2 Novemba 2014 wakati Mama Kanisa alipokuwa anaadhimisha
Siku ya Marehemu wote.
Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kwa ajili ya kuwakumbuka
na kuwaombea marehemu wote waliofariki dunia wakati wa vita, kinzani; kwa wakristo
waliouwawa kikatili kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake bila hata ya kubahatika
kupata Sakramenti za Kanisa au hawakuweza kupata muda wa kusali na kutubu. Amewakumbuka
hata wale ambao hawana mwombezi, watu ambao wamesahaulika kabisa; watu ambao wamefariki
dunia kutokana na baa la njaa na umaskini; watu wambao wamejisadaka kwa ajili ya kutoa
huduma kwa jirani zao.
Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu amewakumbuka wale
wote waliofariki dunia katika kipindi cha mwaka huu, huku wakiwa na imani na matumaini
kwa Yesu Kristo aliyemwaga Damu yake Azizi kwa ajili ya ukombozi wa mwanadamu kutoka
katika lindi la dhambi na mauti. Baba Mtakatifu katika sala yake, anamwomba Mwenyezi
Mungu kutoangalia umaskini, magonjwa na masumbuko ya binadamu, wakati watakapokuwa
wanajongea mbele ya uso wake kwa ajili ya hukumu kwa wenye haki kufurahia maisha ya
uzima wa milele na wadhambi kuingia motoni.
Baba Mtakatifu anamwomba Mwenyezi
Mungu aoneshe uso wenye huruma unaomsindikiza mwanadamu katika hija ya maisha yake,
ili aweze kujitakasa na hatimaye, kupokelewa kwenye huruma ya Mungu isiyokuwa na mwisho.
Anamwomba awaokoe watoto wake wasije wakapotelea kwenye moto wa milele, mahali ambapo
hakuna tena fursa ya kutubu.
Baba Mtakatifu ameziweka roho za waamini marehemu
hasa wale ambao wamefariki dunia bila kupata Sakramenti za Kanisa au kutubu na kumwongokea
Mungu wakati walipokuwa wanakunja maisha yao hapa duniani, mikononi mwa huruma ya
Mungu. Amemwomba Mwenyezi Mungu awajalie watoto wake neema, ili kifo kitakapowadia
kiwakute wanakesha, ili hatimaye, waweze kupata pumziko la milele huko mbinguni.
Baba
Mtakatifu anasema, Siku ya kuwakumbuka Marehemu wote ina uhusiano wa pekee na Siku
kuu ya Watakatifu wote; kama ilivyo furaha na majonzi yaliyojionesha wakati wa maisha
ya Yesu Kristo, muhtasari wa imani na matumaini ya Kikristo. Mama Kanisa anaposafiri
hapa dunia anafurahia maombezi ya Watakatifu na Wenyeheri, wanaosaidia kuenzi utume
wa Kanisa katika utangazaji wa Habari Njema ya Wokovu. Kwa upande mwingine, anashiriki
pia kilio cha watoto wake wanaofariki dunia na hivyo kumshukuru Mungu kwa kuwakomboa
kutoka katika lindi la dhambi na mauti.
Baba Mtakatifu amewakumbuka wale wote
wanaotumia muda wao kwa ajili ya kutembelea Makaburini, mahali ambapo waamini wamelala
usingizi wa amani na wataweza kuamshwa na Yesu Kristo mwenyewe. Kifo cha mwili wa
mwanadamu ni kama usingizi, ndiyo maana Mama Kanisa anawahimiza watoto wake kusali
kwa ajili ya kuwaombea marehemu, lakini kwa namna ya pekee kabisa kwa njia ya maadhimisho
ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, msaada wa pekee ambao unaweza kutolewa na waamini hapa
duniani kwa ajili ya roho za marehemu hasa wale waliosahaulika kama wanavyohimiza
Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, kwa kuonesha umoja katika Fumbo la Mwili
wa Kristo, yaani Kanisa.
Baba Mtakatifu anawahimiza waamini kutunza makaburi
na kuwaombea marehemu, kama kielelezo cha imani na matumaini kwa kutambua kwamba,
kifo si hatima ya maisha ya mwanadamu, kwani mwanadamu ameumbwa ili kupata maisha
ya uzima wa milele yanayopata chimbuko lake kwa Mungu mwenyewe.
Waamini wanahimizwa
kumwomba Bikira Maria aliyeonja mateso ya Mwanaye Yesu Kristo pale chini ya Msalaba,
lakini baadaye akashiriki katika furaha ya Ufufuko wa Mwanaye mpendwa na kwamba, daima
yuko karibu na wote wanaomkimbilia kwa imani na matumaini.
Na Padre Richard
A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.