2014-11-01 11:59:56

Hija ya kiekumene ni endelevu, haipaswi kusimama!


Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox anasema mchakato wa kiekumene kati ya Kanisa Katoliki na Kanisa Kiorthodox hauna budi kuendelezwa na kamwe haupaswi kusimama na kwamba, hii ndiyo changamoto inayofanyiwa kazi kati yake na Baba Mtakatifu Francisko ambaye anatarajiwa kumtembelea mwishoni mwa Mwezi Novemba, 2014 kama sehemu ya maadhimisho ya Siku kuu ya Mtakatifu Andrea.

Hii ni fursa ya kuendeleza mchakato wa majadiliano ya Kiekumene ulionzishwa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican pamoja na viongozi wa Kanisa la Kiorthodox kwa wakati huo. Akizungumza na kundi la waandishi wa habari kutoka Austria, Patriaki Bartolomeo wa kwanza anasema, hakuna mambo makubwa wanayotarajiwa kufanya kati yake na Baba Mtakatifu Francisko atakapomtembelea, bali kwa pamoja watatoa tamko, kama kielelezo cha mwendelezo wa majadiliano ya kiekumene, hija ambayo imefikiwa na Makanisa haya mawili.

Miaka kadhaa iliyopita, Waamini wa Kanisa la Kiorthodox na Kikatoliki walikuwa wanaangaliana kama maadui, lakini hadi sasa kumekuwepo na mabadiliko makubwa yanayopaswa kuendelezwa na kudumishwa kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa la Kristo. Tume ya Kimataifa ya majadiliano inayounganisha wajumbe kutoka Kanisa Katoliki na Kanisa la Kiorthodox, Mwezi Septemba, 2014, wamejadili pamoja na mambo mengine, dhamana na utume wa Askofu wa Roma kwa ajili ya Kanisa la Kiulimwengu. Hapa bado wajumbe wanaendelea kuyafanyia kazi mawazo haya.

Patriaki Bartolomeo wa kwanza anasema, amekuwa na uhusiano wa pekee na Baba Mtakatifu Francisko tangu alipoteuliwa na hatimaye kusimikwa kwake hapo tarehe 19 Mei 2013, ulikuwa ni mwanzo wa ukurasa mpya uliofunguliwa baada ya Makanisa haya mawili kutengana kunako mwaka 1054. Ni ukurasa wa urafiki na udugu katika Kristo, ulioendelea kuimarishwa wakati Baba Mtakatifu Francisko alipotembelea Nchi Takatifu pamoja na ile siku ambayo Baba Mtakatifu na viongozi wakuu wa Serikali na dini kutoka Israeli na Palestina walipokutana mjini Vatican ili kusali kwa ajili ya amani.

Patriaki Bartolomeo wa kwanza anasema, kilele cha hija ya kichungaji ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Uturuki kuanzia tarehe 28 hadi tarehe 30 Novemba 2014 ni hapo Jumamosi ya tarehe 29 Novemba atakapotembelea Jumba la Makumbusho la Sofia, atakapotembelea Msikiti wa Sultan Ahmet na kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Roho Mtakatifu. Viongozi hawa wawili wataongoza Sala ya Kiekumene katika Kanisa la Kipatriaki la Mtakatifu George na baadaye, watateta kwa faragha.

Patriaki Bartolomeo wa kwanza anasema, tangu Mwenyeheri Paulo VI, Yohane Paulo II, Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI ni viongozi ambao wametembelea Kanisa la Kiorthodox na kwa namna ya pekee, viongozi hawa wawili wa mwisho, wamemtembelea mara tu baada ya kuanza utume wao, kuonesha umuhimu wa mchakato wa majadiliano ya kiekumene.

Majadiliano ya kiekumene yanajikita katika maisha ya sala: ukweli na upendo; ni hija endelevu ambayo kamwe haipaswi kusimama kwani inasukumwa na upendo unaomwilishwa kwa njia ya mahusiano ya watu. Hata kama majadiliano ya kiekumene yameendelea kuchukua muda mrefu, lakini mahusiano ya viongozi wa Makanisa haya mawili yamekuwa na kuboreka kwa haraka sana katika kipindi cha miaka kumi iliyopita.

Patriaki Bartolomeo wa kwanza anasema, anayo furaha kubwa kumkaribisha Baba Mtakatifu Francisko nchini Uturuki, ili kushiriki katika maadhimisho ya Siku kuu ya Mtakatifu Andrea, inayoadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 30 Novemba.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.