Sri Lanka inamsubiri Papa Francisko kwa mikono miwili!
Kardinali Malcolm Ranjith, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Colombo nchini Sri Lanka, wakati
akizungumza na Mapadre wa Jimbo lake amethibitisha kwamba, Baba Mtakatifu Francisko
anatazamiwa kutembelea Sri Lanka kuanza tarehe 13 hadi tarehe 15 Januari 2015.
Mapadre
wametakiwa kuwajulisha waamini pamoja na taasisi zinazosimamiwa na kuongozwa na Kanisa
Katoliki, ili kuanza maandalizi ya kina kwa ajili ya ujio wa Baba Mtakatifu Francisko
nchini mwao. Waamini kwa namna ya pekee, wanahimizwa kusali, ili hija hii ya kichungaji
iweze kufanikiwa na kuzaa matunda yanayokusudiwa!
Taarifa zinaonesha kwamba,
kwa sasa Baraza la Maaskofu Katoliki Sri Lanka kwa kushirikiana na Vatican wanaendelea
kukamilisha maandalizi na kwamba, ratiba kamili itakamilika baada ya ujumbe kutoka
Vatican kutembelea nchini Sri Lanka mapema mwezi Novemba. Maaskofu wamekwishazungumza
na vyombo vya ulinzi na usalama, ili kuhakikisha kwamba, ziara hii inafanyika katika
hali ya utulivu na amani.
Mwanzoni, wananchi wengi walionesha wasi wasi wa
kufanyika kwa hija ya kichungaji ya Baba Mtakatifu nchini Sri Lanka kutokana na maendeleo
ya mchakato wa uchaguzi nchini humo, uchaguzi ambao unatarajiwa kufanyika kabla au
baada ya hija ya kichungaji ya Baba Mtakatifu Francisko. Viongozi wa Kanisa wanashauri,
ikiwezekana uchaguzi ufanyike baada ya hija ya kichungaji ya Baba Mtakatifu nchini
Sri Lanka.