2014-10-30 07:46:20

SIRI YA KIFO!


Mpendwa mwana wa Mungu nikikutakia daima furaha na matumaini, ninakualika katika tafakari yetu, tukiwakumbuka marehemu wote. Kila mwaka tarehe 2 Novemba na zaidi sana mwezi mzima wa Novemba ni siku na wakati ambao tunaalikwa kuwakumbuka na kuwaombea marehemu wote. Kwa kawaida siku zote Mama Kanisa haachi kusali kwa ajili ya marehemu, lakini basi siku ya leo ameiweka rasmi iwe ni ya wazi kwa ajili yao yaani Kanisa zima la wateswa lililoko toharani. Huo ndio utajiri wa Kanisa linapogawa mastahili ya msalaba wa Kristu kwa wahitaji walioko safarini kuelekea mbinguni.

Tukitazama vema litrujia kwa ajili ya marehemu wote, jambo la kwanza tunaloalikwa kuliweka mioyoni mwetu ni kuwa maisha yetu ni mafupi ingawa ni mazuri kuliko. Jambo hili linatoka katika kitabu cha Zaburi pale ambapo mwanadamu analinganishwa na nyasi zinazochipua na kuchanua asubuhi na jioni zimekwishanyauka na kukauka. (Zab. 90: 6) Zaidi ya mzaburi, tunaona katika kitabu cha Hekima ya Solomoni mwandishi akisema siku zetu ni kama kivuli kipitacho na tukishakufa hatuwezi kurudi toka humo, tena siku ya kufa kwetu imepangwa na hakuna atakayeweza kuirudisha.

Toka mtiririko wa mawazo haya juu ya maisha kuwa mafupi na juu ya falsafa ya kifo, mwana hekima akisonga mbele, anathubutu kusema “hivyo tujifurahishe kwa chochote kizuri kilichopo, tuvitumie kabisa viumbe kama wakati wa ujana, tujishibishe divai ya thamani na marashi tujichumie maua ya vuli yasitupite, tuache alama za anasa zetu zionekana kila mahali, maana ndivyo maisha yalivyo ndivyo tulivyopangiwa! (Hek. 2: 5-9).

Haya ni mawazo ambayo yaja kwa sababu ilikuwa bado hawajapata kuelewa na kufanya upembuzi juu ya fumbo la kifo, kumbe kilichofuata ni kama kukata tamaa. Hivi leo jambo hilo hujitokeza tena na tena, natumai umesikia mara kadhaa, watu wakisema tuponde mali na kula raha kifo chaja!

Mpendwa, pamoja na mawazo haya yaliyojitokeza katika kitabu cha Hekima ya Solomoni yaani mkato wa tamaa, hakukuwa na njia ya kuzima moja kwa moja hekima ya wale ambao walitaka kujiendeleza katika kutambua umaana wa ufupi wa maisha na pia mwanzo na mwisho wa maisha yenyewe yaliyo zawadi toka kwa Mungu. Kumbe wanamwomba Mungu wakisema, basi “utufundishe ufupi wa maisha yetu ili tuweze kuwa na hekima” (Zab. 90: 12). Hekima waombayo ni ile ya kutambua kuwa wao katika ulimwengu huu ni mahujaji na hivi wanapaswa kuishi na kutumia mali za ulimwengu kwa ajili ya wokovu wao na jirani. Wanatafuta hekima ambayo itawafanya kila mara waonje ile heri maarufu ya kuwa maskini wa roho na hivi kujiweka tayari kwa ajili ya uzima wa milele.

Mpendwa mwana wa Mungu, kifo kwa kawaida ni rafiki yetu tunayeishi pamoja naye. Wachunguzi wa mambo na hasa wanafalsafa wanasema, magonjwa na taabu mbalimbali, dhuruma na mambo kama hayo ni alama zinazopeleka habari daima ili tutayarishe majeshi kwa ajili ya kupigana na kifo na tena ni habari kwamba tutakufa. Ni dokezo ili kujiandaa kwa ajili ya kushindana na kifo na hata kuibuka mshindi kwa kupata zima wa milele.

Alama hizi hutukumbusha kwamba tu mahujaji na hivi tukae tayari. Pamoja na alama hizi, tunaposali katika siku hii ya marehemu wote, hofu bado huja, hata hivyo, lengo la Mama Kanisa si kutuogopesha bali kutuandaa kwa ajili ya kifo na pia kutambua ufupi wa maisha yetu ili tuyaishi kwa hekima na hatimaye tuibukie katika ufufuko na ndio ushindi.

Nabii Isaya katika somo la kwanza anatangaza furaha itakayoletwa na Masiha, Masiha ambaye ni mshindi dhidi ya kifo, na hivi kifo hakiogopeshi bali ni mlango wa kuingilia kwa ajili ya maisha ya ukamilifu, maisha mapya tukimzunguka mwenye sherehe pale mlimani ndiko mbinguni. Katika mtazamo huohuo, Mt Paulo anapowaandikia Warumi anawaambia kitu gani chaweza kututenga na furaha iliyoletwa na Mkombozi wetu? Anasema tumaini letu halijengeki katika kutoa jasho letu, bali katika upendo usio na masharti, yaani upendo upeo na mkamilifu, ndio upendo wa Mungu. Kwa namna hiyo kifo mbele ya Mungu hakina nafasi tena bali ni jambo la kupita!

Mpendwa, katika somo la Injili ya Matayo, Bwana anatualika kumkimbilia yeye ili kutua mizigo na kupumzika katika yeye. Matuzi ya mizigo ni sasa na mapumziko huanza sasa, kumbuka neema unazojaliwa kila siku. Lakini hasa pumziko katika ukamilifu wake ni mbinguni. Ili kuweza kufikia jambo hilo anatualika kuwa watu wenye hekima, anasema kuweni kama watoto wadogo na katika kuwa kama watoto wadogo haimanishi kuchezea udongo bali kuwa na hekima tambuzi ya matendo makuu ya Mungu katika maisha ya kila siku.

Yawezekana kukajitokeza pengine wazo yakwamba anawachukia matajiri na watu wazito, hapana!, bali watu hawa wako karibu na hatari ya kujengeka katika kiburi na wakasahau jambo la unyenyekevu ambalo ni nguzo ya hekima.

Mpendwa, Bwana akisonga mbele anatualika kupembua ni akina nani wanaweza kumjua Mungu? Wa kwanza ni Mwana na wa pili wale ambao Mwana apenda kuwashirikisha hiyo hekima iliyo kuu kuliko zote, yaani Kumjua Mungu Baba. Kwa hakika kumjua Mungu ni kuwa na mang’amuzi kina (deep experience). Katika kundi la pili hatuoni waandishi, sijui wataalamu wala wenye nguvu, bali tu wale apendao kuwamegea hazina hiyo. Hawa kwa hakika ni wale wanaokubali kuwa kama watoto wadogo, ni wale wanaoomba kila siku wakisema utufundishe ufupi wa maisha yetu.

Mpendwa mwana wa Mungu, tukishaweka msingi juu ya kifo ambacho kinaambaa mwishoni mwa maisha mafupi, tunaalikwa tena katika siku ya leo kuungana na Kanisa zima linalojinyenyekesha kuomba huruma ya Mungu kwa ajili ya wahitaji ndio marehemu wote, ndio waliolala toharani wakitakaswa ili waingie mbinguni. Kanisa linatambua ufupi wa maisha ya mwanadamu na kumbe ni lazima litekeleze wajibu wake wa kuishi hekima ya Kimungu.

Ndiyo kusema katika litrujia ya marehemu wote linataka kutangaza kwamba maisha hayapotei bali hubaki na hivi ule muunganiko uliopo kati ya marehemu (kanisa la wateswa), watakatifu wa mbinguni (Kanisa la washindi) na kanisa la wapiganaji ndio sisi huunda kwa pamoja kanisa moja familia ya Mungu.

Fundisho tulilolisikia juu ya umoja wa Kanisa shindi, Kanisa la wateswa na Kanisa la mahujaji linawekwa mbele yetu na Mwenye heri, Papa Paulo VI akisema, “sisi twasadiki ushirika wa waamini wote wa Kristo, wa wale walio bado safarini hapa duniani, wa wale waliokufa ambao wanapata utakaso, wa wale wenye heri ya mbingu, wote pamoja hufanya Kanisa moja tu. Nasi twasadiki kwamba katika umoja huu, mapendo ya huruma ya Mungu na ya watakatifu wake yasikiliza daima sala zetu” (KKK 962) Ndiyo kusema kuwaombea marehemu ni sehemu ya imani yetu, ni upendo kwa jirani tukiitikia Injili ya Bwana ya kumsaidia aliye katika taabu, aliyemhitaji.

Kuwaombea marehemu ni kielelezo kimojawapo cha imani yetu katika ufufuko, kwa maana kama hatusadiki yakuwa Kristu alikufa na kufufuka imani yetu ni bure. Ni kutokana na msingi huo twaamini kwamba wale waliolala usingizi katika Yesu Kristu mfufuka, parapanda ya Mungu ikilia watafufuliwa kwanza nasi tuliosalia tutanyakuliwa kwa kuwafuata wao.

Kuwaombea marehemu ni jambo la thamani na la imani ambalo si la leo bali limekuwepo katika safari ya wokovu. Tunasoma daima katika kitabu cha pili cha Wamakabayo kuwa Yuda kiongozi wa Wayahudi alichanga fedha kwa kila mtu jumla drakma mbili elfu, akazipeleka Yerusalemu kutoa sadaka ya dhambi. Kwa kufanya hivi alitenda vema na kwa haki kwa kuwa aliukumbuka ufufuo wa wafu. Alifanya hili kwa sababu ya imani na kama asingekuwa na imani kuwa wafu watafufuliwa ingekuwa upumbavu na kazi bure kuwaombea marehemu. (Rej. 2Wak. 12: 43-45).

Basi ndugu yangu mpendwa ninakualika katika msingi uleule wa imani katika ufufuko, kusali daima sala hii “raha ya milele uwape Ee Bwana na mwanga wa milele uwaangazie wapumzike kwa amani, amina”. Ni Sala ya kujenga urafiki na marehemu walioko toharani na hatimaye watakatifu wa mbinguni. Ni sala ambayo yatukumbusha marehemu wapendwa Wakristu wenzetu na hata wasio wakristu, ambao wengine tuliwafahamu kwa karibu na hivi yatudai wajibu wa kuomba huruma ya Mungu kwa ajili yao pasipo kukoma. Huruma hiyo isiyo na mwisho twadaiwa kuiomba katika unyenyekevu unaojifungamanisha na sala yetu.

Mama Kanisa ametuwekea Misa tatu kwa ajili ya marehemu wote, ili kwa njia hiyo marehemu wapate msaada wa masitahili ya Kristu kwa njia ya sadaka yake ya msalabani. Anataka asiwepo hata mmoja atakayekosa huruma na msaada wa Mungu. Katika Misa hizi tatu Injili zagusa Heri Nane, njia ya utakatifu na habari ya ufufuko wa wafu, lililotumaini letu na imani yetu tunaposafiri kuelekea ukamilifu, yaani, uzima wa milele ambao huja baada ya kifo. Tunasali na kutumaini kuwa, kwa kifo maisha hayaondolewi ila hugeuzwa na kuwa maisha mapya, maisha makamilifu (rejea utangulizi wa Wafu I).

Basi mpendwa mwanatafakari, leo ni wakati wa kusali na kuwatembelea waliolala kule makaburini ili muunganiko katika sala ukamilishwe katika upendo unaoonekana katika maisha yetu. Yafaa pia kufunga kidogo kwa ajili ya wapendwa wetu ili kuisimika sala yetu katika majitoleo ya Kristu mteswa na hatimaye uibuke na ushindi wa Kristu mfufuka. Kumbukeni pia kujiombea wewe mwenyewe kwa maana kwakukumbusha kujitayarisha kwa ajili ya safari ya kugeuzwa na kuingia maisha mapya, maisha ya mbinguni. Tumsifu Yesu Kristo.

Tafakari hii imeletwa kwako na Padre Richard Tiganya, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.