2014-10-29 10:33:19

Tanzania kuwa mlango wa bidhaa kutoka Vietnam


Tanzania imekubali ombi la Jamhuri ya Kisoshalisti ya Vietnam kuwa mlango wa kuingiza bidhaa za nchi hizo hasa za mashine na vyakula katika soko la nchi wanachama wa Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC) ambazo kwa sasa uwezo wa nchi hizo kutengeneza mashine siyo mkubwa sana.

Aidha, Tanzania imesema kuwa itaunga mkono jitihada za Vietnam kupata nafasi ya kuwa mjumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UN) asiye wa kudumu na asiye na kura ya turufu. Tanzania pia imesisitiza msimamo wake kuwa iko mbioni kufungua ubalozi nchini Vietnam kama namna ya kukuza na kuimarisha uhusiano mzuri ulioko kati ya nchi hizo, uhusiano ulioanza tokea miaka ya 1960, wakati Vietnam inapigana vita ya kujikomboa. Mwakani, uhusiano wa kibalozi wa Tanzania na Vietnam utatimiza miaka 50 tokea kuanzishwa kwake.

Tanzania ilitoa ahadi hizo Jumatatu, Oktoba 27, 2014 wakati wa mazungumzo rasmi kati ya nchi hizo mbili yaliyofanyika ikiwa ni sehemu ya ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Vietnam. Rais Kikwete ambaye alikuwa katika ziara rasmi ya Kiserikali ya siku mbili katika Jamhuri ya Kisoshalisti ya Vietnam kwa mwaliko wa Rais Truong Tan Sang, amemaliza ziara yake Jumanne, Oktoba 28, 2014.

Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika kwenye Kasri ya Kirais mjini Hanoi, mji mkuu wa Vietnam, Rais Sang alitoa maombi kadhaa kwa Tanzania yenye nia ya msingi ya kuimarisha uhusiano wa kidugu wa miaka mingi kati ya nchi hizo mbili ikiwa ni pamoja na kuisaidia Vietnam kufungua soko muhimu la EAC hasa kwa bidhaa za mashine na vyakula.

Akijibu hoja na maombi hayo ya Rais Sang, Rais Kikwete amesema: “Tutaiunganisha Vietnam na masoko ya nchi za Jumuia ya Afrika Mashariki. Na kuhusu nafasi ambazo Vietnam inaziwania katika UN na katika Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) tutawaunga mkono pia kwa sababu sera yetu ya miaka yote ni kuunga mkono marafiki zetu katika masuala ya kimataifa.”

Kuhusu ombi la Vietnam kuitaka Tanzania kufungua ubalozi nchini humo, Rais Kikwete amesema kuwa uamuzi wa kufanya hivyo, kimsingi, ulikwishakuchukuliwa lakini utekelezaji wake umekuwa unachelewa kwa sababu ya ufinyu wa bajeti. “Kwa kweli Ubalozi wa Vietnam uko kwenye mipango yetu na ucheleweshaji unatokana na watu wa fedha. Lakini jambo la kutia moyo ni kwamba tumeanza tena kufungua balozi zetu ambazo tulikuwa tumezifunga huko nyuma kwa sababu ya matatizo ya bajeti. Tayari, kwa mfano, tumefungua Ubalozi wa Uholanzi. Hivyo, Mheshimiwa Rais, tuwe na subira, mambo yatakwenda vizuri,” alisema Rais Kikwete.

Rais Kikwete pia ametaka kuimarishwa kwa uhusiano kati ya nchi hizo mbili hasa katika maeneo ya maendeleo ya kilimo cha mpunga. “Haja yetu kubwa hasa ni kujifunza kutoka Vietnam namna ya kuendeleza kilimo cha mpunga. Tumepata kulizungumza hili huko nyuma na tukakubaliana, sasa nadhani tuanze kutekeleza.” Rais Sang alikubaliana na hoja hiyo ya Rais Kikwete.

Rais Kikwete amesema ni muhimu kuendeleza ipasavyo kilimo cha mpunga kwa sababu ya kujihakikishia usalama wa chakula cha Tanzania yenyewe na majirani zake lakini zaidi kwa sababu Mpango wa Pili wa Maendeleo utaelekeza nguvu zake katika uzalishaji mkubwa wa kilimo na uanzishaji wa viwanda.

Rais Kikwete pia ameitaka Vietnam kuisaidia Tanzania katika eneo la uzalishaji la kuanzisha Maeneo Maalum ya Uchumi kwa ajili ya kuongeza uwezo wa Tanzania kuuza bidhaa nyingi zaidi kuliko ilivyo sasa. Jumanne, Oktoba 28, 2014, Rais Kikwete ambaye aliitembelea Vietnam kwa mara ya kwanza akiwa Rais, ameweka shada la maua kwenye Kumbukumbu ya Mashujaa wa Kitaifa na Mashuhuda wa Taifa la Vietnam na akaweka shada la maua kwenye Kaburi la Hayati Rais Ho Chi Minh, Kiongozi wa Mapinduzi ya Vietnam.

Aidha, Rais Kikwete alifungua mkutano wa wafanyabiashara wa Tanzania na Vietnam, ambao uliandaliwa kwa pamoja na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na Chama cha Wafanya Biashara na Wenye Viwanda wa Vietnam cha Chamber of Commerce. Baadaye Rais Kikwete alitembelea kiwanda cha vyakula na hasa Samaki cha Trung Son Hung Yen Foodstuff Corporation kinachoajiri wafanyakazi 1,600 na kusindika kiasi cha tani 12,000 za minofu ya samaki kwa mwaka ambazo zinauzwa katika masoko ya nje na hasa Marekani, Japan, Ufaransa, Australia na Norway.

Bwana Nguyen An Hung, Meneja Mkuu wa Kiwanda hicho, alimwambia Rais Kikwete kuwa kiwanda huzalisha na huuza nje minofu ya Samaki yenye thamani ya dolaza Marekani kati ya Milioni 55 na 60 kwa mwaka. Rais Kikwete pia alitembelea Makao Makuu ya Kampuni ya Viwanda vya Nguo vya Garment 10 Corporation (Garco 10), kampuni ambayo ilianzisha kiwanda chake cha kwanza mwaka 1946 na kwa sasa kinaajiri wafanyakazi 10,000.

Rais Kikwete aliambiwa kuwa awali kiwanda hicho kilianzishwa na Jeshi la nchi hiyo na wakati wa vita vya ukombozi kuanzia mwaka 1954, kiwanda hicho kilipewa jukumu la kushona sare za Jeshi. Hata hivyo, baadaye kilifanywa kiwanda cha umma kabla ya kubinafsishwa.

Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni hiyo, Bwana Vu Duc Giang amemwambia Rais Kikwete kuwa kwa sasa Kampuni hiyo ina viwanda 10 katika Vietnam na mbali na kutoa nafasi za ajira kwa wafanyakazi wake, Kampuni hiyo pia hutoa huduma ya elimu ya awali bure kwa watoto wa wafanyakazi, matibabu ya bure kwa wafanyakazi na familia zao na elimu ya juu ya shughuli za uzalishaji na ushonaji nguo kwa wafanyakazi wa viwanda hivyo.

Kabla ya kumaliza ziara yake na kuanza safari ya kurejea nyumbani, Rais Kikwete alikutana na kufanya mazungumzo na Mwenyekiti (Spika) wa Bunge la Jamhuri ya Kisoshalisti ya Vietnam, Mheshimiwa Nguyen Sinh Hung katika ofisi za Bunge mjini Hanoi.








All the contents on this site are copyrighted ©.